Nyanyake mtahiniwa wa KCSE aliyepatikana ameuawa Meru akataa kuzika mwili bila kichwa

Polisi bado hawajafanikiwa kupata kichwa cha marehemu.

Muhtasari

•Mwili wa Beatrice Gatwiri ambao ulikuwa umekatwa kichwa ulipatikana katika eneo la milima ya Rwerea mnamo Januari 13.

•Chepkwony amesema washukiwa wawili ambao wako kizuizini wanasaidia katika uchunguzi wa kifo cha marehemu.

crime scene
crime scene
Image: MAKTABA

Mwanafunzi wa miaka 18 ambaye aliondoka nyumbani baada ya kumaliza KCSE mwezi uliopita alipatikana akiwa amefariki katika eneo la Tigania Central,  Kaunti ya Meru.

Mwili wa Beatrice Gatwiri ambao ulikuwa umekatwa kichwa ulipatikana katika eneo la milima ya Rwerea mnamo Januari 13.

Alikuwa ameondoka nyumbani mnamo Desemba 24 mwaka jana na kwenda kuishi na mpenzi wake aliyetambulishwa kama Allan Kirimi punde baada ya kukamilisha mtihani wake wa kidato cha nne. 

Marehemu alikuwa akiishi na nyanya yake kabla ya kugura nyumbani.

Polisi ambao wanaendelea kutia juhudi katika kutegua kitendawili cha kifo cha mwanadada huyo tayari wamemkamata mpenzi wa marehemu na mwanamume mwingine aliyeuona mwili huo msituni.

Hata hivyo, bado hawajafanikiwa kupata kichwa cha marehemu ambacho kilikuwa kimetenganishwa na mwili. 

Taarifa iliyorekodiwa na polisi inasema kwamba Gatwiri hakukaa na mpenzi huyo wake kwa muda mrefu baada ya kuhamia kwake kwani alioondoka na kugundulika kuwa amekufa siku chache baadaye. 

Bosi wa Polisi katika kaunti ya Tigania ya Kati Joel Chepkwony amesema washukiwa wawili ambao wako kizuizini wanasaidia katika uchunguzi wa kifo cha marehemu.

Mkuu huyo wa polisi hata hivyo ameelezea wasiwasi akisema kuwa umma umekataa kutoa ushirikiano mzuri katika uchunguzi wa mauaji hayo ya kinyama.

Sasa ametoa wito kwa umma na viongozi wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama katika kutafuta kichwa cha marehemu.

Imeripotiwa kuwa nyanyake Gatwiri sasa amekataa kuzika mwili wa mjukuu huyo wake bila kichwa akisema hawezi kupata amani baada ya kufanya hilo na huzuni inaweza kumuandama hadi kufa.