Seneti yaidhinisha mswada wa marekebisho wa IEBC

Maseneta 28 walipiga kura kuunga mkono Mswada wa IEBC (Marekebisho) wa 2022 ambao unabadilisha muundo wa jopo la uteuzi

Muhtasari
  • Kamati hiyo ilikuwa imependekeza kupunguza nafasi zinazotolewa kwa Tume ya Huduma za Bunge (PSC)
SPIKA AMASON KINGI
Image: EZEKIEL AMING'A

Bunge la Seneti limeidhinisha Mswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (Marekebisho) wa 2022, na kutoa njia ya kuajiri makamishna wapya.

Bunge la Seneti lilipitisha mswada huo bila marekebisho baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria Hillary Sigei kuondoa mapendekezo yake ya marekebisho.

Kamati hiyo ilikuwa imependekeza kupunguza nafasi zinazotolewa kwa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) katika jopo la uteuzi kutoka mbili hadi moja na kuongeza zile za Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Siasa hadi mbili kutoka moja.

Maseneta hao pia walikataa marekebisho ya Seneta mteule Catherine Mumma ambaye alinuia kuondoa nafasi iliyotolewa kwa tume ya Utumishi wa Umma na kuichangia kwa Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Kisiasa.

Maseneta 28 walipiga kura kuunga mkono Mswada wa IEBC (Marekebisho) wa 2022 ambao unabadilisha muundo wa jopo la uteuzi ambalo sasa litakuwa na wanachama 2 wanaoungwa mkono na Tume ya Huduma za Bunge.

Tume ya Utumishi wa Umma itatoa mwakilishi mmoja huku LSK ikimfuata mtu mmoja kwenye jopo hilo na baraza la dini mbalimbali litawafuatia wajumbe wawili.

Tume hiyo iliachwa bila makamishna baada ya muda wa Mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna; Boya Molu na Abdi Guliye kustaafu Jumanne, Januari 17 baada ya kuhudumu kwa miaka sita kama ilivyoainishwa na katiba.