KCSE 2022:Watahiniwa 1,146 wapata alama ya A

Mnamo 2022, watahiniwa 841,416 walifanya mitihani ya KCSE kutoka sehemu tofauti za nchi,

Muhtasari
  • Machogu alisikitika kuwa mgomo ulioandaliwa katika Shule ya Wasichana ya St. Francis Mang'u ulikaribia kutatiza shughuli zoezi hilo
WAZIRI WA ELIMU EZEKIEL MACHOGU
Image: ANDREW KASUKU

Jumla ya watahiniwa 1,146 waliofanya mtihani wa KCSE mwaka jana walipata alama ya A.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitangaza matokeo ya mtihani wa KCSE siku ya Ijumaa, Januari 20, katika Mitihani House, Nairobi.

Waziri alisema kwamba watahiniwa 1,146 walipata alama ya A ikilinganishwa na 1,138 katika mtihani wa mwaka wa 2021.

Mwaka 2022, jumla ya watahiniwa 841,416 walifanya mtihani wa KCSE kutoka, uliyofanywa kati ya Desemba 2 na Desemba 23.

Akizungumza katika ukumbi wa Mitihani House, Machogu alibainisha kuwa serikali iliamua kutoa matokeo ya mitihani mapema ili kuwaruhusu wanafunzi hao kujiandaa kwa ajili ya mabadiliko ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

"Kama nilivyosema watahiniwa 841,416 walifanya mtihani wa KCSE 2022 ikilinganishwa na watahiniwa 826,807 wa 2021," Machogu alisema.

Machogu aliwapongeza walimu na watahiniwa, akibainisha kuwa masomo 17 yalipata matokeo mazuri yaliyoimarika ikilinganishwa na masomo 11 mwaka wa 2021.

Machogu alisikitika kuwa mgomo ulioandaliwa katika Shule ya Wasichana ya St. Francis Mang'u ulikaribia kutatiza shughuli zoezi hilo.

Hata hivyo, aliapa kuwaongezea malipo na kushughulikia lalama zao.

"Ninakumbuka kero iliyorekodiwa katika kituo kimojawapo ambapo maafisa wa mitihani walitishiwa kutatiza zoezi hilo," Machogu alisema.

"KNEC hata hivyo iliweza kujibu hilo kuhakikisha zoezi hilo linaendelezwa bila vikwazo. Kwa wakati huu, nataka kuwahakikishia kuwa walifanya kazi ya kupongezwa," Machogu alisema.