Mvulana wa miaka 14 akamatwa baada ya kumsukuma mzee wa miaka 64 hadi kifo

Walioshuhudia walisema mshukiwa alimsukuma marehemu, akateleza na kuanguka chini akigongwa kichwa chake.

Muhtasari

•Mvulana huyo alizuiliwa na polisi baada ya mashahidi kusema kuwa alimsukuma Stanley Githongo, 64 hadi chini na kusababisha kifo chake.

•Polisi wamesema wanachunguza tukio hilo.

Pingu
Image: Radio Jambo

Mvulana mwenye umri wa miaka 14 anachunguzwa baada ya kudaiwa kumsukuma hadi kumuua mzee wa miaka 64 katika eneo la Mowlem, Nairobi.

Mvulana huyo alizuiliwa na polisi baada ya mashahidi kusema kuwa alimsukuma Stanley Githongo, 64 hadi chini na kusababisha kifo chake baada ya mabishano siku ya Jumapili alasiri.

Githongo na wenzake walikuwa na shughuli nyingi katika eneo la ujenzi huku wakiondoa vifaa wakati mvulana huyo akiendesha baiskeli karibu na eneo hilo.

Kulingana na mashahidi, kwa usalama wa mvulana huyo, Githongo alimuonya dhidi ya kupanda karibu walipokuwa wakisukuma vifaa nje.

Hili lilizua ugomvi kati ya kijana na marehemu.

Hapo ndipo marehemu alipompiga kofi mvulana huyo akimwambia akae mbali na eneo hilo.

Walioshuhudia walisema mvulana huyo kwa kujibu alimsukuma marehemu, akateleza na kuanguka chini akigongwa kichwa chake.

Githongo alilala bila fahamu kwa muda kabla ya kukimbizwa katika hospitali ya Mama Lucy ambapo alifikwa na mauti.

Polisi wamesema wanachunguza tukio hilo.

Walisema wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa maiti kuashiria jinsi mtu huyo alifariki kabla ya kuchukua hatua zaidi.