Jamaa akamatwa baada ya kumchinja nyanyake Mombasa

Mwili wa Shariffa Ali Salim, 80 ulipatikana umetapakaa kwenye dimbwi la damu nyumbani kwake

Muhtasari

• Maafisa hao walichukuwa silaha ya muuaji kutoka eneo la tukio kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu kwenye chumba cha kuhifadhia.

Shariffa Ali Salim ambaye aliuawa katika nyumba yake mjini Mombasa mnamo Januari 21.
Shariffa Ali Salim ambaye aliuawa katika nyumba yake mjini Mombasa mnamo Januari 21.

Hali ya swintofahamu inazingira kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 20 anadaiwa kumchinja nyanyake katika eneo la Mji wa Kale, kaunti ya Mombasa.

Mwili wa Shariffa Ali Salim, 80 ulipatikana ukiwa umetapakaa kwenye dimbwi la damu nyumbani kwake Jumapili usiku muda mfupi baada ya tukio hilo.

Familia ya marehemu ilisema mshukiwa aliyetambulika kwa jina la Abdulaziz All Swaleh aligombana na nyanyake ndani ya nyumba hiyo kabla ya kuchukua kisu cha jikoni na kumkata shingoni.

Waliokuwepo walidai mshukiwa alitaka pesa kutoka kwa ajuza huyo na alipokataa kutoa pesa, jamaa huyo alikasirika na kumdunga kisu.

Msaidizi wa nyumbani ambaye alikuwa ndani ya nyumba alijaribu kumwokoa bila mafanikio.

Polisi walisema waliitwa eneo la tukio baada ya mshukiwa kukamatwa na wananchi alipokuwa akijaribu kutoroka.

Maafisa hao walichukuwa silaha ya muuaji kutoka eneo la tukio kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kusubiri upasuaji wa maiti na uchunguzi zaidi.

Kamanda wa polisi wa Pwani Titus Karuri alisema wanamhoji mshukiwa huyo kwa taarifa zaidi kuhusu mauaji hayo ya kinyama.

"Haya yanaonekana kuwa mauaji na wataalamu wanalichunguza. Tunataka kuelewa sababu iliyochochea mauaji hayo,” alisema.

Shariffa Ali Salim ambaye aliuawa katika nyumba yake mjini Mombasa mnamo Januari 21.
Shariffa Ali Salim ambaye aliuawa katika nyumba yake mjini Mombasa mnamo Januari 21.