Uhuru aongoza mawaziri wa zamani kutembelea familia ya marehemu Magoha

Uhuru aliwateua mawaziri wa zamani Fred Matiang’i na Raphael Tuju kuunda kamati ya kusaidia maandalizi ya mazishi.

Muhtasari

• Rais Mustaafu alitoa wito kwa waliokuwa mawaziri waliohudumu na Marehemu Magoha kuhudhuria mazishi yake, eneo la Yala kaunti ya Siaya.

Rais Mustaafu Uhuru Kenyatta akitoa rambirambi zake alipowasili nyumbani kwa aliyekuwa waziri George Magoha. 1/31/2023
Rais Mustaafu Uhuru Kenyatta akitoa rambirambi zake alipowasili nyumbani kwa aliyekuwa waziri George Magoha. 1/31/2023
Image: WILFRED NYANGARESI

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amezuru nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa elimu marehemu George Magoha ili kufariji familia.

 Uhuru siku ya Jumanne aliongoza waliokuwa mawaziri katika serikali yake kuipa pole familia ya Magoha ambaye alihudumu kama waziri wa elimu katika serikali yake. 

Image: WILFRED NYANGARESI

Rais mustaafu alikuwa ameandamana na mkewe mama Margaret Kenyatta alipowasili nyumbani kwake Magoha na kupokelewa na aliyekuwa waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa.  

Mawaziri wa zamani waliondamana na Uhuru walikuwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiangi, Ukur Yattani (Hazina), Eugene Wamalwa (Ulinzi), Joe Mucheru (ICT), Margaret Kobia (Utumishi wa Umma na Jinsia) na aliyekuwa katibu wa kudumu katika wizara ya Mambo ya Ndani Karanja Kibicho. Pia alikuwepo kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka. 

Baadhi ya mawaziri waliohudumu na marehemu Magoha katika serikali ya Uhuru na ambao walitembelea familia ya Magoha. 1/31/2023.
Baadhi ya mawaziri waliohudumu na marehemu Magoha katika serikali ya Uhuru na ambao walitembelea familia ya Magoha. 1/31/2023.
Image: WILFRED NYANGARESI

Rais Mustaafu alitoa wito kwa waliokuwa mawaziri waliohudumu na Marehemu Magoha kuhudhuria mazishi yake, eneo la Yala kaunti ya Siaya. Rais mustaafu aliwateua waliyokuwa mawaziri Fred Matiang’i na Raphael Tuju kuunda kamati ya kusaidia katika maandalizi ya mazishi. 

Marehemu Magoha ambaye atazikwa Februari 11 alikuwa miongoni mwa mawaziri wachapa kazi katika serikali ya Uhuru Kenyatta.

Atakumbukwa sana kwa kudhibiti udanganyifu katika mitihani ya kitaifa na kuongoza uzinduzi wa mtaala mpya wa elimu wa CBC.