Hatima ya Kuhuzunisha! Wanandoa wa Nakuru waliojaliwa watoto 5 wawapoteza wote

"Mwisho wa kusikitisha. RIP kwa malaika watano," Njoki alisema

Muhtasari

•Habari hizo za kuhuzunisha zilifichuliwa na mbunge wa eneo la Bahati, Irene Njoki siku ya Alhamisi asubuhi.

•Watoto hao watano walizaliwa wakiwa na miezi sita na ilibidi wawekwe kwenye incubator ili waweze kuishi

•Watoto hao, wasichana wanne na mvulana mmoja walikuwa na uzito wa kati ya gramu 500 na 650 walipozaliwa.

Margaret Wairimu ambaye alijifungua Quintuplets katika mrengo wa Mama na Mtoto wa Margaret Kenyatta katika Hospitali ya Nakuru Level 5.
Margaret Wairimu ambaye alijifungua Quintuplets katika mrengo wa Mama na Mtoto wa Margaret Kenyatta katika Hospitali ya Nakuru Level 5.
Image: LOICE MACHARIA

Watoto wachanga wote watano wa dereva wa Nakuru Simon Ndung'u Kinyajui ,28, na mke wake Margaret Wangui ,25, wamaeaga dunia.

Habari hizo za kuhuzunisha zilifichuliwa na mbunge wa eneo la Bahati, Irene Njoki siku ya Alhamisi asubuhi.

"Mwisho wa kusikitisha. RIP kwa malaika watano,"  Njoki alisema kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Haya yanajiri masaa machache baada ya mbunge huyo kuwazadi wanandoa hao kwa baraka ya kushangaza waliyopokea.

"Kuzaliwa kwa mtoto siku zote huchukuliwa kuwa baraka kutoka kwa Mungu, Simon ndungu na Margaret Wangui walitembelewa kutoka mbinguni baada ya kupokea watoto watano," Njoki alisema siku ya Jumatano.

Timu ya mbunge huyo iliwatembelea wanandoa hao hospitalini na kuwatunuku zawadi kemkem baada ya Bi Wangui kujifungua.

Afisa Msimamizi wa Matibabu wa Hospitali ya Nakuru Level 5, Aisha Maina alisema Margaret Wairimu mwenye umri wa miaka 25 alijiwasilisha katika kituo hicho akiwa mjamzito mnamo Januari 29.

"Alikuja kupitia eneo la  wagonjwa wa nje wa hospitali akiwa hana raha na walipomchunguza, madaktari waligundua kuwa alikuwa na mimba ya watoto wengi," Maina alisema.

Alisema mwanadada huyo alilazwa kwa uangalizi kwa sababu alikuwa na ujauzito uliozingirwa na hatari.

Maina alisema maumivu hayo yalizidi, na kuwalazimu madaktari kufanya upasuaji wa dharura ili kuwaokoa mama na watoto.

"Watoto hao walizaliwa wakiwa na miezi sita na ilibidi wawekwe kwenye incubator ili waweze kuishi," alisema.

Maina alisema watoto hao, wasichana wanne na mvulana mmoja walikuwa na uzito wa kati ya gramu 500 na 650 walipozaliwa.

Mama yuko katika hali dhabiti na ataruhusiwa kurudi nyumbani pindi tu watoto wachanga watakapofikia uzani unaofaa.

Wanandoa hao wenye umri wa maka wana mtoto mwingine wa miaka 4.