Mama Ngina Kenyatta avunja kimya kuhusu madai ya kukwepa ushuru

Alielezea kusikitishwa kwake na jinsi jina la familia yake lilivyochafuliwa jina kuhusu suala la ushuru.

Muhtasari

•Mama Ngina, bila kutaja majina, alionekana kushangazwa na ripoti zinazodai kuwa familia yake ilikwepa kulipa kodi.

•Aliendelea kuthubutu serikali kupiga mnada mali yake iwapo atabainika kuwa amekosa kutekeleza wajibu wake wa ushuru.

Rais Uhuru akisalimiana na Mama Ngina Kenyatta katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo Oktoba 20, 2015
Rais Uhuru akisalimiana na Mama Ngina Kenyatta katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo Oktoba 20, 2015
Image: REUTERS

Aliyekuwa Mke wa Rais, Mama Ngina Kenyatta amemjibu Rais William Ruto na washirika wake kuhusu madai kuwa familia yake imekuwa ikikwepa ushuru kwa kipindi ambacho mwanawe Uhuru Kenyatta alikuwa mamlakani.

Katika video zilizofikia Radio Jambo, Mama Ngina, bila kutaja majina, alionekana kushangazwa na ripoti zinazodai kuwa familia yake ilikwepa kulipa kodi.

Mama Ngina, ambaye alikuwa akihutubia kanisa moja Lamu, alielezea kusikitishwa kwake na jinsi jina la familia yake lilivyochafuliwa jina kuhusu suala la ushuru.

Mke huyo wa Rais wa zamani alisema utaratibu unaostahili wa sheria ufuatwe katika kushughulikia suala hilo badala ya kuchafua majina ya watu.

"Hakuna haja ya kuharibia wengine majina na mimi ndio watu wasikike wanafanya kazi. Hapana, Mtu ashtakiwe, alipe kile anatakiwa kulipa," Mama Ngina alisema.

Aliendelea kuthubutu serikali kupiga mnada mali yake iwapo atabainika kuwa amekosa kutekeleza wajibu wake wa ushuru.

Mama Ngina alisema mashambulio yaliyofanywa dhidi ya familia yake si ya haki na ni ya uongo na hivyo kutoa changamoto kwa serikali kuwa wazi kuhusu suala hilo badala ya kufanya siasa.

"Na Kama ni mimi, hata kama sijalipa kwa mwaka mmoja, mali ichukuliwe ilipe ushuru kwa sababu ni lazima. Hakuna haja ya kufanya kazi ya kisiasa ya hapa na kule. Na Si kweli kwamba sijalipa ushuru. Na watu wanajua hawasemi ukweli," aliongeza.