Kindiki amtahadharisha Raila kuhusu maandamano ya nchini kote

Odinga ameandaa misururu ya mikutano katika kaunti mbalimbali huku akiwahamasisha wafuasi kukataa utawala wa Rais William Ruto.

Muhtasari
  • Akihutubia wanahabari ambapo alitoa kadi yake ya siku 100 ofisini, CS Kindiki alisema kuwa serikali haitaingilia shughuli za upinzani, mradi hazitavuruga biashara au kukinzana na sheria
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI
Image: KWA HISANI

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki Jumatatu alionya kiongozi wa Azimio La Umoja Raila Odinga kwa kuvunja sheria katika mikutano yake inayoendelea nchini kote.

Odinga ameandaa misururu ya mikutano katika kaunti mbalimbali huku akiwahamasisha wafuasi kukataa utawala wa Rais William Ruto.

Tayari amefanya mikutano mitatu jijini Nairobi.

Akihutubia wanahabari ambapo alitoa kadi yake ya siku 100 ofisini, CS Kindiki alisema kuwa serikali haitaingilia shughuli za upinzani, mradi hazitavuruga biashara au kukinzana na sheria.

“Sina shughuli na wale wanaofanya maandamano; kwa kweli sijali, kwa sharti moja; kwamba wanashika sheria na utaratibu. Siku watakapojaribu kuvunja sheria, kuvunja amani, kuchochea fujo za umma, ndiyo siku ambayo uzito kamili wa Wizara ya Mambo ya Ndani utawajia,” alionya Kindiki.

"Wanaweza kufanya mikutano ya hadhara, wanaweza kuchokonoa na kuandamana, mradi tu wasivuruge biashara na kuwalazimisha watu ambao hawako sawa nao kuwasikiliza kwa nguvu ... wanaweza kufanya siasa zao ... hiyo sio kazi yangu."

Aliongeza kuwa serikali haitasita kumfungulia mashtaka mwanasiasa yeyote anayejishughulisha na shughuli zinazotatiza usalama nchini.

“Nimewaambia wanasiasa wote, ni marafiki na washirika wangu wanaponisaidia kuifanya Kenya kuwa nchi salama. Mara tu wanapoleta tishio kwa matarajio hayo wao ni wateja wangu kwa maana nyingine,” CS alisema.

Odinga, ambaye alishindwa na Ruto katika kinyang’anyiro cha urais uliokuwa na ushindani mkali Agosti mwaka jana, anashikilia kuwa kura hizo zilivurugwa na kumpendelea naibu huyo wa rais wa zamani.