Jopo maalum lapendekeza kufurushwa kwa Jaji Juma Chitembwe

Walalamishi walimshtumu jaji huyo kwa kula mlungula katika kitika mzozo ardhi

Muhtasari

• Mwenyekiti wa Jopo hilo Jaji Mumbi Ngugi akimpokeza rais ripoti siku ya Jumanne alisema jopo hilo lilimpata jaji huyo na hatia ya utovu wa nidhamu.

Rais William Ruto amepokea ripoti ya jopo maalum lililoundwa kuchunguza mienendo ya Jaji wa Mahakama Kuu aliyesimamishwa kazi Said Juma Chitembwe.

Mwenyekiti wa Jopo hilo Jaji Mumbi Ngugi akimpokeza rais ripoti siku ya Jumanne alisema jopo hilo lilimpata jaji huyo na hatia ya utovu wa nidhamu.

“Jopo kwa kauli moja lilipata kuwa jaji Chitembwe alikiuka Katiba wakati akitekeleza majukumu yake,” alisema Jaji Ngugi.

Rais Ruto alishukuru jopo hilo kwa kuharakisha kazi yake, akibainisha kuwa uongozi huja na uwajibikaji.

Kiongozi wa taifa alisema Katiba inasalia kuwa sheria zinazoongoza kwa wale wote ambao wamepewa jukumu la kuwahudumia Wakenya.

“Ninataka kuwakumbusha Wakenya kwamba kuna mbinu za kushughulikia jambo lolote ambalo mtu anaaminika kutenda kinyume na sheria alipokuwa akitekeleza majukumu ya umma,” alisema Rais Ruto.

Rais alisema atatekeleza mapendekezo ya jopo hilo.

“Nitafanya kile ambacho Katiba inatarajia kutoka kwangu,” alisema Rais.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alimsimamisha kazi Jaji Chitembwe mwaka jana na kuunda jopo maalum kuchunguza madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya jaji huyo.

Wanachama wengine wa jopo hilo walikuwa Wakili Fred Ojiambo, Jaji Abida Ali Aroni, Jaji Nzioki wa Makau, James Ochieng’ Oduol, Jenerali Mstaafu Jackson Ndung’u na Dkt Lydia Nzomo.

Maombi manne yaliwasilishwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, Francis Wambua, Imgrad Geige na David Leboo Ole Kilusu wakitaka Jaji huyo aondolewe afisini.

Walalamishi hao walimshtumu jaji huyo kwa kula mlungula katika kitika mzozo ardhi ambao alishughulikia kama jaji.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO.