Jalang'o afichua kwa nini alilazimika kukubali mwaliko wa rais Ruto kutembelea ikulu

Jalang'o alisema alikuwa akifuatilia nyumba za bei nafuu katika wadi ya Highrise.

Muhtasari

•Jalang'o alisema walioalikwa hawakujadili siasa bali miradi ya maendeleo katika eneo bunge lake.

•Mkutano huo ulipata upinzani kutoka kwa chama cha ODM,

na Mbunge wa Langata Phelix Odiwour katika Ikulu Februari 7, 2023
Rais William Ruto na Mbunge wa Langata Phelix Odiwour katika Ikulu Februari 7, 2023
Image: PSC

Mbunge wa Langa'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o amesema aliitwa na Rais William Ruto kwa mkutano katika Ikulu siku ya Jumanne.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, Jalang'o alisema walioalikwa hawakujadili siasa bali miradi ya maendeleo katika eneo bunge lake.

“Wakati Rais alitembelea eneo langu kwa mara ya kwanza kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, nilimpigia simu kiongozi wa chama changu, Baba akaniambia, kama ni maendeleo, endelea na uwe sehemu yake,” alisema.

Jalang'o pia alisema Kiongozi wa ODM Raila Odinga amewapa wanachama wa chama hicho ufunguo wa kufanya kazi na Ruto kuleta maendeleo.

"Nilikuwa nikivuma jana, lakini tulikuwa wabunge tisa, timu iliyokuwepo ilifuatilia kila mradi ambao Ruto alikuwa ameahidi watu wa Nyanza," alisema.

Akitumia ukurasa wake wa Twitter y Jumanne baada ya mkutano huo, Jalang'o alisema alikuwa akifuatilia nyumba za bei nafuu katika wadi ya Highrise.

"Leo, tulipata kifungua kinywa na Rais, nilifuatilia tarehe ya Kuanza kwa ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika wadi ya Highrise na kukamilika kwa TVET ya Langata," alisema.

Mkutano huo ulipata upinzani kutoka kwa chama cha ODM, huku mkurugenzi wa mawasiliano Philip Etale akisema kuwa mkutano wa wabunge hao haukuwashangaza.

"Chama kimekuwa kikifuatilia kwa karibu shughuli za nyuma ya pazia zinazohusisha baadhi yao na leo ilikuwa kilele tu," alisema katika taarifa yake.