Mbunge Salasya aonekana na mwenzake Linet Toto baada ya kutishia kumtunga mimba

Salasya alibainisha kuwa Mungu alikuwa na sababu ya kumfanya yeye na Toto kuwa wabunge.

Muhtasari

•Wawili hao walikuwa miongoni mwa wageni wengi ambao walihudhuria mkutano wa ibada wa Nabii David Awuor katika uwanja wa Bomet mnamo Februari 19.

•Mbunge huyo wa muhula wa kwanza mwenye utata mwingi alionyesha picha kadhaa akiwa na Toto zilizopigwa kwenye hafla hiyo.

walikutana katika uwanja wa Bomet siku ya Jumapili, Februari 19.
Wabunge Peter Salasya na Linet Toto walikutana katika uwanja wa Bomet siku ya Jumapili, Februari 19.
Image: TWITTER// PETER SALASYA

Mbunge wa Mumias East Peter Salasya na Mwakilishi wa Wanawake wa Bomet Linet Toto walikutana siku ya Jumapili.

Wanasiasa hao vijana ambao hivi majuzi walihusika katika mzozo wa siasa walikuwa miongoni mwa wageni wengi ambao walihudhuria mkutano wa ibada wa Nabii David Awuor katika uwanja wa Bomet mnamo Februari 19.

Akizungumza wakati wa ibada hiyo kubwa, Salasya alibainisha kuwa Mungu alikuwa na sababu ya kumfanya yeye na Toto kuwa wabunge. 

Kuna sababu Mungu aliamua kutuchagua sisi vijana tusiokuwa na pesa za kufanya kampeni kama mimi na Mhe Linet Toto hapa, na mbunge wa Chepalungu. Alijua tutaweza kuendelea na uamsho huu," alisema.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza mwenye utata mwingi alionyesha picha kadhaa akiwa na Toto zilizopigwa kwenye hafla hiyo.

"Siku ya mafanikio na yenye baraka nilipojiunga na maelfu ya maelfu ya waumini wa Huduma ya Toba katika Uwanja wa Bomet," alisema.

Mbunge huyo aliendelea kuwalika viongozi wa kanisa hilo katika eneo bunge lake la Mumias ili kuendeleza injili.

Wawili hao walivuma wiki jana baada ya Salasya kumkosoa Toto kwa kumshambulia kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa matamshi makali.

"Alianza 1997 kabla ya mimi kuzaliwa. Alikuja 2002, 2007, 2017, na sasa 2022. Daima amekuwa akidai ushindi wake wa urais umeibiwa," Toto alimsuta Raila.

Toto alimweleza Raila kuwa Rais William Ruto alichaguliwa kihalali na wananchi wa Kenya wakati wa uchaguzi wa Agosti mwaka jana.

Mbunge Peter Salasya alishindwa kuficha ghadhabu yake kufuatia matamshi ya mwakilishi wa wanawake huyo na akachukua hatua ya kumjibu katika mkutano wa kisiasa uliofanyika mjini Busia mnamo Februari 12.

Salasya alimuonya Toto akisema atampa ujauzito kwa kutomheshimu kiongozi wa muungano wa Azimio la One Kenya.

"Alafu wale vijana vidogo ambao wanatusi Baba, kuna kengine kalichaguliwa kama hakana pesa kama Peter Salasya kanaitwa Toto. Kanaongea ati kwa Baba, ntakaweka mimba huko wiki ijayo" alisema Salasya.

Baadaye hata hivyo alifutilia mbali matamshi yake na kusema,  "Kweli, msichana wenu mdogo kwa kweli amefanya kiheshima, hongera @LinetChepkorir_, sasa sitafanya kile kitu lakini kwa heshima tu kidogo kwa baba Raila na tutakuwa marafiki wakubwa tena sana...All the best harusi lazima nikuje sasa."