Chuo kikuu cha Meru kufunguliwa tena Jumatano

Sherehe ya mahafala iliyopangwa kufanyika Machi 11 pia itaendelea kama ilivyopangwa.

Muhtasari

• Hatua ya kukifungua tena chuo hicho imetokana na kurejeshwa kazini Naibu Chansela mkuu wa chuo hicho Profesa Romanus Odhiambo.  

WAZIRI WA ELIMU EZEKIEL MACHOGU
Image: ANDREW KASUKU

Chuo Kikuu cha Meru kimetangaza kufunguliwa tena siku Jumatano baada ya kufungwa kutokana na fujo za wanafunzi siku chache zilizopita. 

Hatua ya kukifungua tena chuo hicho imetokana na kurejeshwa kazini Naibu Chansela mkuu wa chuo hicho Profesa Romanus Odhiambo.  

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu siku ya Jumanne aliagiza kurejeshwa kazini mara moja kwa Prof. Odhiambo ili chuo hicho kufunguliwe na kuandaa hafla ya kufuzu baadye wiki hii. 

Taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa baraza la uongozi wa Chuo hicho Bosire Mwebi ilisema kwamba hatua ya kumteua kaimu Naibu Chansela umebatilishwa na Prof. Odhiambo atarejea ofisini. 

Wanafunzi wa Meru University waandamana kufuatia kufurushwa kwa VC Odhiambo.
Image: HISANI

"Baraza litafanikisha kujea kwa Prof. Odhiambo ofisini mara moja kabla ya mwisho wa tarehe 7 Machi, 2023," alisema. 

Baraza hilo lilisema kwamba chuo hicho kitaruhusu wanafunzi kurejea chuoni ifikiapo Jumatano, Machi 8 ili shughuli za kawaida kurejelewa. 

Sherehe ya mahafala iliyopangwa kufanyika Machi 11 pia itaendelea kama ilivyopangwa. 

Prof. Odhiambo alitumwa kwa likizo ya kustaafu na baraza la uongozi kwa misingi kwamba hakuweza kuafikia matarajio katika majukumu yake.