Wizara ya fedha yatangaza zabuni kudhibiti mende na panya

wizara ilisema hati za zabuni zinaweza kupakuliwa bila malipo kwenye tovuti yake.

Muhtasari

• Ni sera ya serikali kwamba asilimia 30 ya zabuni zitolewe kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. 

Mende
Mende
Image: HISANI

Hazina ya Kitaifa imetangaza zabuni za huduma za ufukizaji na udhibiti wa wadudu wakiwemo panya, fursa ambayo imetengwa kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu pekee. 

Katika tangazo lililolipiwa, wizara ilisema hati za zabuni zinaweza kupakuliwa bila malipo kwenye tovuti yake. 

"Zabuni hii imetengewa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu pekee," lilisema tangazo hilo.

Hati za zabuni zilizokamilishwa zitapelekwa kwenye Jengo la Hazina mnamo au kabla ya tarehe 21 Machi 2023, saa tano mchana. 

"Zabuni zitafunguliwa mara moja mbele ya wazabuni au wawakilishi wao waliowachagua kuhudhuria ufunguzi katika Jengo la Hazina saa tano asubuhi saa za Kenya," wizara ilisema. 

Serikali imekuwa ikifanya juhudi za makusudi kushughulikia kwa dhati matatizo ya vijana kuanzia ukosefu wa ajira, umaskini na ujuzi usiotumika.  

Ni sera ya serikali kwamba asilimia 30 ya zabuni zitolewe kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. 

Sera hiyo inatekelezwa katika muktadha wa Mpango wa Upatikanaji wa Fursa za Ununuzi Serikalini (AGPO) ambao ulizinduliwa rasmi na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Oktoba 16, 2013. 

AGPO imeegemezwa kwenye Kifungu cha 227 cha Katiba kuhusu ununuzi wa bidhaa na huduma wa umma wenye usawa, wa uwazi na wa gharama nafuu.Pia inatokana na Kifungu cha 55 cha mwaka 2010 kuhusu hatua za uthibitisho na Sheria ya Ununuzi wa Umma na Uondoaji wa Mali, 2015.

Lengo la programu ya AGPO ni kuwezesha makampuni yanayomilikiwa na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuweza kushiriki katika fursa za Serikali.