Afueni kwa Matiang'i baada ya DPP kukataa mashtaka dhidi yake

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, ODPP aliagiza DCI kufunga faili ya uchunguzi bila hatua nyingine za polisi.

Muhtasari
  • Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aligundua kuwa ushahidi uliotolewa haukutosha kuendeleza mashtaka
Fred Matiang'i
Fred Matiang'i
Image: HISANI

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i hatashtakiwa kortini kutokana na kuchapishwa kwa habari kuhusu madai ya kuvamiwa na polisi katika nyumba yake ya Karen mnamo Februari 8.

Hii ni baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kusema kuwa ushahidi uliotolewa na Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) dhidi ya Matiang’i na Wakili wake Danstan Omari hautoshi kuendeleza mashtaka hayo.

“Baada ya uchambuzi huru na wa kina wa ushahidi uliotolewa na uhakiki wa maelezo ya mashahidi, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aligundua kuwa ushahidi uliotolewa haukutosha kuendeleza mashtaka yaliyotajwa hapo juu dhidi ya Dkt. Fred Okeng’o Matiang’i na wakili Bw. Danstan Omari. Ushahidi uliotolewa haukukidhi viambajengo vinavyohitajika kuthibitisha kila kosa lililotajwa kama inavyotakiwa kisheria,” ODPP alisema.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, ODPP aliagiza DCI kufunga faili ya uchunguzi bila hatua nyingine za polisi.

DCI ilikuwa imetuma faili kwa DPP kukagua na kupendekeza kufunguliwa mashtaka kwa wawili hao kwa makosa ya; Kula njama za kutenda kosa kinyume na kifungu cha 393 cha Kanuni ya Adhabu na Uchapishaji wa taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 23 cha Sheria ya Kompyuta na Matumizi Mabaya na Makosa ya Mtandao namba 5 ya mwaka 2018.