Kanisa na Msikiti zateketezwa huku makundi hasimu yakilaumiana Kibera

Bosi wa polisi alisema mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa katika matukio hayo.

Muhtasari

•Na katika tukio la kulipiza kisasi, kundi la vijana lilivamia kanisa la PCEA katika eneo hilo na kulichoma moto.

•Na jioni, vijana wenye hasira walitembea hadi kwenye kanisa la PCEA karibu na msikiti na kuichoma moto.

moto
Moto moto
Image: PICHA YA MAKTABA

Sehemu ya msikiti katika mtaa wa Kibera iliteketezwa wakati wa ghasia ambazo zilishuhudiwa katika eneo hilo huku kukiwa na madai ya uhalifu uliofadhiliwa.

Na katika tukio la kulipiza kisasi, kundi la vijana lilivamia kanisa la PCEA katika eneo hilo na kulichoma moto.

Vibanda vingine kadhaa vilivyo karibu na msikiti na kanisa vilibomolewa wakati wa ghasia hizo za Jumatatu usiku.

Kizaazaa kilianza wakati kundi moja liliposhambulia kibanda kimoja karibu na msikiti huo ambao uko katika eneo la Makina. Kibanda hicho kilidaiwa kuwa makao ya kundi lililokuwa likifadhili mashambulizi yao.

Kulingana na polisi, katika harakati hizo, kundi hilo lilichoma kibanda hicho.

Polisi walisema moto ulisambaa hadi katika msikiti ulio karibu na kuteketeza sehemu fulani yake kabla ya wazima moto na waumini waliokuwa wamekwenda huko kuswali kuudhubiti.

Kumekuwa na mapigano kati ya polisi na kundi ambalo lilikuwa likilenga kioski hicho.

Hili lilihitimisha maandamano ya awali katika eneo hilo huku baadhi ya wenyeji wakisema polisi walikuwa wamezingira mtaa huo na hawakuwa wanamruhusu mtu yeyote kuondoka.

Polisi waliingilia kati na kutawanya kundi lililolenga kioski.

Na jioni, vijana wenye hasira walitembea hadi kwenye kanisa la PCEA karibu na msikiti na kuichoma moto.

Sehemu kubwa ya jengo hilo ilibomolewa huku vijana wakipigana huku wengine wakijaribu kuuzuia moto huo, walioshuhudia walisema.

Gari la zima moto lilifika eneo la tukio dakika chache baadaye na kufanikiwa kuzuia kuenea kwa moto huo.

Mkuu wa polisi wa Kilimani Muturi Mbogo alisema hakuna vifo vilivyoripotiwa wakati wa machafuko hayo.

Alisema polisi wanachunguza matukio hayo.

Mbogo alisema mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa katika matukio hayo.

Mvutano uliendelea kuwa juu katika eneo hilo usiku kucha na kulikuwa doria chache za polisi.

Maafisa walisema kulikuwa na mkutano wa waandishi wa habari uliopangwa katika eneo hilo Jumanne utakaoandaliwa na viongozi kutoka msikiti na kanisa.

Polisi walisema machafuko hayo yaliendelea hadi kwenye njia ya kuelekea Kusini ambapo kundi lilifunga barabara hiyo yenye shughuli nyingi kwa saa nyingi.

Hii iliathiri trafiki hadi usiku wa manane.

Siku ya Jumanne, wenyeji walikuwa wakihesabu hasara huku waathiriwa wakitafuta usaidizi wa kujenga upya miundo iliyoathiriwa.