Raila alaani uvamizi wa shamba la rais mstaafu Uhuru Kenyatta

Bw Odinga alisema hajahusika na uharibifu wa mali na waandamanaji.

Muhtasari

•Kiongozi huyo wa upinzani alisema anaamini shambulio hilo lilitekelezwa na ‘majangili’ waliokodishwa na serikali.

•Anasema ni bahati mbaya kwamba waandishi wa habari walilengwa na polisi na waandamanaji wakati wa maandamano ya Jumatatu.

KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amelaani uvamizi wa mali ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Uhuru Kenyatta.

Katika mahojiano na BBC, kiongozi huyo wa upinzani alisema anaamini shambulio hilo lilitekelezwa na ‘majangili’ waliokodishwa na serikali.

Bw Kenyatta ni mshirika wa Odinga. Jumatatu ilikuwa siku ya pili ya maandamano dhidi ya serikali yaliyoitishwa na Bw Odinga kwa madai kwamba kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi uliopita pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

Kuporwa kwa shamba kubwa la Bw Kenyatta kunaonekana kama kulipiza kisasi hatua yake ya kumuunga mkono Bw Odinga.

Maandamano zaidi yanapangwa, siku ya Alhamisi wiki hii. Lakini serikali imelaani ghasia na usumbufu unaosababishwa na maandamano hayo.

Bw Odinga aliambia BBC kuwa hajahusika na uharibifu wa mali na waandamanaji, na alitetea haki ya kikatiba ya kuandamana.

Anasema ni bahati mbaya kwamba waandishi wa habari walilengwa na polisi na waandamanaji wakati wa maandamano ya Jumatatu.

Baadhi ya watu walitoka shambani wakiwa wamebeba kondoo mabegani mwao
Baadhi ya watu walitoka shambani wakiwa wamebeba kondoo mabegani mwao
Image: BBC

Alikosoa baadhi ya sera za kiuchumi za Rais William Ruto akisema ingawa gharama ya maisha ni tatizo la ulimwengu wote, nchi nyingi zimejaribu kuwaokoa raia wao kutokana na mdororo wa kiuchumi, lakini utawala wa Ruto umeondoa ruzuku na wananchi wanateseka zaidi sasa.

Bw Odinga alisema yuko tayari kukutana na Rais Ruto kwa mazungumzo lakini akataja masharti mawili yanayohitaji kuafikiwa. Kwanza, seva za uchaguzi za kielektroniki zifunguliwe ili kuthibitisha ikiwa kura ya mwaka jana iliibiwa na pili kwamba uteuzi wa makamishna wapya wa tume ya uchaguzi unapaswa kuhusisha pande zote.

Mahakama Upeo ya Kenya ilitupilia mbali kesi ya Odinga kupinga kushindwa kwake katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana, lakini bado anasisitiza kuwa uamuzi huo uliathiriwa.

Bw Odinga alisema yuko tayari kukutana na Rais Ruto kwa mazungumzo lakini akataja masharti mawili yanayohitaji kuafikiwa.
Bw Odinga alisema yuko tayari kukutana na Rais Ruto kwa mazungumzo lakini akataja masharti mawili yanayohitaji kuafikiwa.
Image: BBC

Uvamizi dhidi ya mali ya Uhuru na Raila

Katika wiki ya pili ya maandamano dhidi ya serikali palitokea visa viwili vya uharibifu wa mali zinazohusihwa na Odinga na rais wa zamani Uhuru Kenyatta.Watu wasiojulikana walivamia kampuni ya East Africa Spectre Limited katika barabara ya Mombasa na kuharibu mali.

Kampuni hiyo ni ya utengenezaji na usambazaji wa mitungi ya gesi inahusishwa na familia ya Raila Odinga.

Meneja wa ulinzi na usalama katika kampuni hiyo Humphrey Waswa aliviambia vyombo vya habari kuwa takriban watu 50 walifika kwenye kampuni hiyo wakiwa kwenye pikipiki mwendo wa saa saa tano unusu asubuhi na kuwashambulia.

“Walikuwa wakisaidiwa na magari manne ambayo hayakuwa na nambari za usajili, Land cruiser na tunashuku kuwa lengo lao lilikuwa ni mkurugenzi wetu mkuu kwa sababu ofisi yake ndiyo imeharibika sana,” alisema.

Waswa alisema kampuni itatoa taarifa za kina baadaye baada ya uchunguzi kufanyika na kuhitimishwa.

Image: bbc

Hakukuna aliyejeruhiwa wakati wa tukio hilo.

Katika tukio jingine jana,watu wasiojulikana walivamia shamba linalomikiwa na familia ya Kenyatta na kukata miti pamoja na kutoroka na mifugo.Baadaye wakati wa siku moto mkubwa ulizuka katika ardhi hiyo kwenye barabara ya mkato ya Eastern Bypass katika kaunti ya Kiambu inayopakana na mji mkuu Nairobi .

Kampuni ya maziwa ya Brookside Dairy, na shule ya Peponizipo ndani ya ardhi hiyo kubwa .Hakuna tamko lililotolewa na polisi kuhusu matukio yote mawili .