Afisa wa polisi aliyejeruhiwa wakati wa maandamano Kisumu afariki

Afisa huyo akiwa ameandamana na wengine walizidiwa nguvu na waandamanaji waliokuwa wamezua ghasia.

Muhtasari

• Baada ya polisi kuzidiwa nguvu, waandamanaji walivamia Jamia Supermarket na kuharibu na kuiba bidhaa dukani.

Jamia Supermarket ambapo afisa wa polisi Ben Oduor alijeruhiwa na waandamanaji siku ya Alhamisi, Machi 30. Picha: FAITH MATETE
Jamia Supermarket ambapo afisa wa polisi Ben Oduor alijeruhiwa na waandamanaji siku ya Alhamisi, Machi 30. Picha: FAITH MATETE

Afisa wa polisi aliyeruhiwa wakati wa maandamano ya Muungano wa Azimio katika kaunti ya Kisumu amefariki.

Kulingana na ripoti ya polisi, afisa Ben Oduor wa kituo cha polisi cha Keroka huko Nyamira ambaye alikuwa akishika doria wakati wa maandamano mjini Kisumu alijeruhiwa katika eneo la Jamia Supermarket.

Afisa huyo akiwa ameandamana na wengine walizidiwa nguvu na waandamanaji waliokuwa wamezua ghasia.

Alikimbizwa kwa matibabu katika hospitali ya Aga Khan ambapo alifariki Alhamisi usiku akiwa katika chumba cha ICU.

Mwili wake unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Wakati wa kisa cha Alhamisi baada ya maafisa hao kuzidiwa nguvu, waandamanaji walivamia duka hilo kuu, kuharibu na kuiba bidhaa dukani.

Mmiliki wa duka hilo Hussein Hassan alikuwa na machungu akihoji alichokuwa amewafanyia waandamanaji kiasi cha kudhalilishwa hivyo.

Hassan alisema alipoteza bidhaa zenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

"Nina familia na watu wanaonitegemea na sijui nianzie wapi," alisikika akisema.

TAFSIRI: DAVIS OJIAMBO.