Mfanyikazi mwanamke katika Chicken Inn afariki kazini baada ya kudungwa kisu na mpenziwe, Kitengela

Mashahidi walidai mshukiwa alimvamia mwanamke huyo baada ya kubaini kuwa alikuwa akimsaliti kimapenzi.

Muhtasari

•Polisi na mashahidi walisema kisa hicho kilitokea siku ya Ijumaa usiku katika jumba lenye shughuli nyingi la Chicken Inn karibu na kituo cha mafuta.

•Polisi walisema hawakuwa wamegundua nia ya kitendo hicho lakini walishuku kuwa mzozo wa mapenzi ndio sababu.

CRIME
Image: MAKTABA

Mfanyikazi wa kike katika mkahawa wa vyakula vya haraka wa Chicken Inn, Kitengela alifariki baada ya kudungwa kisu na mwenzake wa kiume.

Polisi na mashahidi walisema kisa hicho kilitokea siku ya Ijumaa usiku katika jumba lenye shughuli nyingi la Chicken Inn karibu na kituo cha mafuta.

Kulingana na walioshuhudia, mwanamume huyo ambaye hakuwa zamu aliingia kwenye mkahawa huo Ijumaa usiku mwendo wa saa mbili unusu usiku na kumdunga mwanamke huyo mara kadhaa kwa kisu.

Mashahidi wengine walisema walisikia mayowe na zogo ndani ya mgahawa huo na walipochunguza walimwona mwanamume akiwa na kisu akimshambulia mwanamke huyo.

Polisi walisema hawakuwa wamegundua nia ya kitendo hicho lakini walishuku kuwa mzozo wa mapenzi ndio sababu.

"Mshambuliaji amekuwa nje ya kazi lakini alijitokeza na kumvamia mwanamke huyo na wenzake wanadai kuwa wawili hao walikuwa wapenzi," afisa wa polisi katika eneo la tukio alisema.

Umati wa watu waliokusanyika katika eneo la tukio walimvamia mwanamume huyo kabla ya polisi kufika kuokoa maisha yake.

Mshukiwa huyo ambaye alipata majeraha makubwa kutoka kwa kipigo cha kitutu aliokolewa na polisi waliomkimbiza katika hospitali ndogo ya Kaunti ya Kitengela.

Baadhi ya mashahidi pia walidai kuwa mwanamume huyo alimvamia mwanamke huyo baada ya kubaini kuwa alikuwa akimsaliti kimapenzi.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi ukiendelea kwani eneo hilo lilikuwa limefungwa kwa ajili ya kusafishwa.

Huku hayo yakijiri, mshukiwa wa wizi aliponea kifo kwa chupuchupu baada ya kupigwa na kundi la watu katika eneo la Athi River.

Walioshuhudia walisema mshukiwa alikamatwa baada ya kudaiwa kunaswa akiiba mahindi kwenye shamba la kando ya barabara eneo hilo.

Tukio la Jumamosi asubuhi lilishuhudia umati wenye hasira ukimpiga mshukiwa kwa mateke na makofi.

Polisi wanakataza watu kuwapiga washukiwa na kusema kuwa ni uhalifu. Wanataka washukiwa wafikishwe kwa polisi ili washughulikiwe.