Aliyekuwa mwenyekiti IEBC Issack Hassan aeleza kwa nini alitaka Raila ashinde urais 2013

Hassan alibainisha kuwa ilikuwa wakati wa huzuni kwake alipomtangaza Uhuru kuwa mshindi.

Muhtasari

•Akizungumza Jumatano, Hassan alisema hii ni kwa sababu ya uhusiano wake na Waziri Mkuu huyo wa zamani wakati huo.

•Aliongeza kuwa angetaka pia Wakenya wapate urais wa Raila Odinga.

Raila Odinga akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan.
Raila Odinga akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan.
Image: MAKTABA

Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan amefichua kwamba alitamani Raila Odinga ashinde uchaguzi wa urais wa Machi 2013.

Akizungumza Jumatano, Hassan alisema hii ni kwa sababu ya uhusiano wake na Waziri Mkuu huyo wa zamani wakati huo.

Alibainisha kuwa Raila alichangia pakubwa katika kuibuka kwake kuwa mkuu wa tume la uchaguzi, licha ya baadhi ya watu kujaribu kuhujumu uteuzi wake kama mwanachama wa Tume ya Kupitia Katiba.

“Ninamheshimu sana waziri mkuu na katika kazi yangu ya kwanza kama kamishna wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, alikuwa mwenyekiti wa kamati teule ya bunge kuhusu katiba, walituhoji na mimi nilikuwa miongoni mwa waliochaguliwa kutoka eneo la Kaskazini Mashariki. Hilo ni jambo moja ambalo huwa nampa sifa kwa sababu kulikuwa na majaribio ya kujaribu kuingilia uteuzi wetu lakini alikataa," Hassan alisema.

Aliongeza kuwa angetaka pia Wakenya wapate urais wa Raila Odinga.

Hili hata hivyo alisema sivyo kwani alimtangaza Uhuru Kenyatta (mstaafu) kuwa mshindi.

Hassan alibainisha kuwa ilikuwa wakati mbaya kwake, lakini haya yalikuwa mapenzi ya watu wa Kenya na hakuwa na chaguo.

“Nilikuwa mwenyekiti wa IIEC kwa uungwaji mkono wake kisha IEBC kwa uungwaji mkono wake.Kama kuna mtu ninayemheshimu na kumshukuru ni yeye na kwa kweli ningetamani ashinde uchaguzi na kuwa rais wetu kwa sababu tulihitaji kuonja urais wake. .

"Kama mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, nilitangaza tu matakwa ya wananchi. Ilikuwa wakati mgumu sana kwangu, lakini unaweza kufanya nini?" Alisema kwenye Citizen TV.

Kufuatia matokeo hayo, Raila na washirika wake walianza mashambulizi dhidi ya tume hiyo yakiwemo maandamano kote jijini Nairobi wakitaka watimuliwe.