Upande wa mashtaka waomba Mackenzie aendelee kukaa kizuizini kwa siku 60 zaidi

Kufikia sasa miili ya watu zaidi ya 243 imeshafanyiwa upasuaji katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi katika Kaunti ya Kilifi.

Muhtasari
  • Katika ombi la kutaka kuongezewa muda, upande wa mashtaka unasema  bado haujahitimisha uchunguzi na wanahitaji muda zaidi.
Mchungaji Paul Mackenzie

Pasta wa kanisa la Good News International Paul Mackenzie amefikishwa katika Mahakama ya Shanzu jijini Mombasa leo Ijumaa, Juni 2, 2023. ambapo upande wa mashtaka unaomba aendelee kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi.

Katika ombi la kutaka kuongezewa muda, upande wa mashtaka unasema  bado haujahitimisha uchunguzi na wanahitaji muda zaidi.

"Kurudishwa rumande kwa muda wa siku 60 ni muda mdogo zaidi unaowezekana ambao upelelezi unaweza kukamilika chini ya mazingira yaliyopo na ni njia ndogo zaidi za kudumisha Uadilifu wa upelelezi dhaifu," zinasoma karatasi za mahakama.

Wanadai kuwa hakuna mabadiliko ya hali ya kuachiliwa huru kwa Mackenzie na washukiwa wengine 17 tangu uamuzi wa mahakama hiyo Mei 10 waliporudishwa rumande.

"Bado kuna sababu za msingi za kuwanyima dhamana hadi upelelezi ukamilike na kuna uwezekano mkubwa wa mashtaka makubwa dhidi ya washukiwa," zinasoma hati za mahakama.

Kufikia sasa miili ya watu zaidi ya 243 imeshafanyiwa upasuaji katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi katika Kaunti ya Kilifi.

Wengi ni wale ambao miili yao iliondolewa kwenye makaburi ambayo maafisa wa usalama walipata msituni Shakahola.