Mauaji Siaya: Mwanamke amuua mamake na bintiye na kumdunga mpenziwe Kabla ya Kujiua

Atieno anashukiwa kukosana na mpenziwe Kennedy Onyango, 35, kulingana na maafisa wa polisi.

Muhtasari

• Majirani walipata mwili wa mamake kwenye dimbwi la damu pamoja na mjukuu wake, ambaye alikuwa na majeraha kadhaa ya panga.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ndogo ya Bondo kaunti ya Siaya wanachunguza kisa ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 30 anadaiwa kuwaua bintiye na mamake, kumjeruhi vibaya mpenziwe, kisha kujitoa uhai katika kijiji cha Nyangera Kambajo Jumanne usiku. 

Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Macrine Atieno anadaiwa kumuua bintiye mwenye umri wa miaka 10 na mama yake Perez Anyango (60) kabla ya kwenda nyumbani kwa mpenzi wake kumshambulia na kumjeruhi vibaya kabla ya kurejea nyumbani na kujinyonga. 

Atieno anashukiwa kukosana na mpenziwe Kennedy Onyango, 35, kulingana na maafisa wa polisi. Majirani walipata mwili wake ukining'inia juu ya mti kwenye nyumba ya babake, walipoingia ndani ya nyumba kumjulisha mamake walishtuka kuona mwili wa mamake kwenye dimbwi la damu pamoja na mjukuu wake, ambaye alikuwa na majeraha kadhaa ya panga. 

Naibu chifu wa eneo hilo alisema pia walipokea ripoti kuwa mpenzi wake pia alikuwa katika hali mbaya baada ya kushambuliwa kwa panga.  Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.