Gachagua avunja kimya kuhusu bei ya juu ya mafuta

Alieleza kuwa serikali inafahamu na inajali changamoto zinazowakabili Wakenya kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Muhtasari
  • Alieleza kuwa ni fursa nzuri kuwahudumia Wakenya na kwa hivyo, viongozi hawafai kuwa wazembe na kuwadharau watu.
Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa KICC alipoongoza nchi kuadhimisha Siku ya Ushirika,
DP Gacjagua Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa KICC alipoongoza nchi kuadhimisha Siku ya Ushirika,
Image: PCS

Naibu Rais Gachagua Jumapili alivunja kimya chake kuhusiana na ongezeko la bei ya mafuta iliyotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA).

Gachagua, akitoa kauli yake ya kwanza baada ya kuwasili nchini kutoka kwa safari ya kikazi nchini Colombia, alieleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni suala la kimataifa na kuwataka Wakenya kuwa na subira huku serikali ikijitahidi kutatua suala hilo.

“Kwa heshima kubwa, ningependa kuwasihi watu wa Kenya kufahamu kwamba suala la bei ya mafuta ni changamoto duniani kote. Mambo yatakuwa mazuri tunapoendelea," DP alisema.

Alieleza kuwa serikali inafahamu na inajali changamoto zinazowakabili Wakenya kutokana na gharama ya juu ya maisha.

"Rais William Ruto anaendelea kujitolea kutafuta suluhu za kudumu na endelevu kwa changamoto za kiuchumi zinazokabili taifa letu kuu," aliahidi.

Aliendelea kuwakemea Makatibu wa Baraza la Mawaziri na washauri ambao wameshutumiwa kwa kutojali changamoto zinazowakabili Wakenya.

Naibu Waziri wa Biashara, Moses Kuria na mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Rais William Ruto David Ndii, alibainisha kuwa maoni yao yalikuwa ya kizembe na hayawakilishi wadhifa rasmi wa serikali au wa Rais William Ruto.

Gachagua alifichua kuwa hata alipokuwa nje ya nchi, alikuwa akifuatilia kesi na kutilia shaka busara katika njia ambayo viongozi hao wawili wamechukua kushughulikia suala hilo nyeti.

Alieleza kuwa ni fursa nzuri kuwahudumia Wakenya na kwa hivyo, viongozi hawafai kuwa wazembe na kuwadharau watu.

“Humtaji mwajiri wako kwa kiburi. Fanya hivyo kwa unyenyekevu na adabu,” Gachagua alishauri.