Mudavadi akutana na mawaziri kabla ya mazungumzo na mfalme Charles III

Msururu wa mazungumzo yamepangwa kati ya Mfalme na Mawaziri wa Serikali jijini Nairobi.

Muhtasari

•Mkutano huo ambao pia uliwaleta pamoja makatibu wa baraza la mawaziri ulikuja kabla ya mazungumzo ambayo yamepangwa na Mfalme Charles III na Malkia Camilla.

Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi akiwa na mawaziri wakati wa mkutano katika Hoteli ya Serena, Nairobi mnamo Oktoba 31, 2023. Picha: X
Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi akiwa na mawaziri wakati wa mkutano katika Hoteli ya Serena, Nairobi mnamo Oktoba 31, 2023. Picha: X

Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi alifanya mkutano wa baina ya nchi mbili Jumanne na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza anayeshughulikia, Jumuiya ya Madola na Maendeleo.

Mkutano huo ambao pia uliwaleta pamoja makatibu wa baraza la mawaziri ulikuja kabla ya mazungumzo ambayo yamepangwa na Mfalme Charles III na Malkia Camilla.

"Tulijadiliana kuhusu masuala mbalimbali, yanayohusu wizara na idara zote za serikali yetu," Waziri wa Ulinzi Aden Duale alisema.

Kuhusu Ulinzi, Duale alisema walichunguza masuala kadhaa yanayogusa mkataba wa ushirikiano wa ulinzi uliopo tayari, makubaliano ya kukabiliana na ugaidi na vituo vya waasi kati ya nchi hizo mbili.

Mafunzo na uundaji wa vikosi maalum vya baharini na njia zinazowezekana za kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu pia yalijadiliwa, alisema.

Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na baadhi ya makatibu wakuu miongoni mwa maafisa wengine wa Uingereza pia walihudhuria.

Msururu wa mazungumzo yamepangwa kati ya Mfalme na Mawaziri wa Serikali jijini Nairobi.

Mfalme huyo ambaye ameambatana na Malkia Camilla aliwasili nchini Jumatatu usiku.

Wanandoa hao wa kifalme wako nchini kwa Ziara ya Kiserikali ya siku nne.

Walipokelewa na Rais William Ruto na Mkewe Mama Rachel Ruto katika Ikulu ya Nairobi Jumanne asubuhi.