Watano wajeruhiwa katika makabiliano baina ya polisi na mshukiwa, Nairobi

Polisi walifanikiwa kumuua mshukiwa huyo alipovumani kwa nyumba ya mpenzi wake

Muhtasari

•Polisi walisema Samuel Karui alikuwa anasakwa kwa msururu wa wizi wenye vurugu na matukio ya mauaji ndani ya Kasarani na mazingira yake

•Mpenzi wa mshukiwa huyo alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa uchunguzi zaidi

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Takriban watu watano walilazwa  hospitalini   wakiwa na majeraha baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na mshukiwa anayesakwa.

Waathiriwa waliolazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta walipata majeraha mbali mbali baada ya nyumba zao kumiminiwa risasi wakati mshukiwa wa wizi aliyekuwa akisakwa alipigwa risasi na kuuawa katika majibizano ya risasi katika eneo la Githurai, Nairobi.

Polisi walisema Samuel Karui almaarufu Sammy Steppa alisakwa kwa msururu wa wizi, vurugu na matukio ya mauaji katika eneo la Kasarani na viungani mwake.

Alikabiliwa  na polisi katika nyumba ambayo ilisemekana kuwa ya mpenzi wake wakati alipokuwa amemtembelea.

Polisi walisema kuwa mwenzake alifanikiwa kutoroka ingawa walipata bastola. Kamanda wa polisi Nairobi Adamson Bungei alisema wanachunguza tukio hilo.

“Tutafuatilia suala hilo,Waliojeruhiwa hali zao zinaendelea vizuri hospitalini," alisema.

Mpenzi wa mshukiwa huyo alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa uchunguzi zaidi.

Mwezi uliyopita, afisa wa polisi alipigwa risasi na kuuawa huku wengine watatu wakijeruhiwa katika makabiliano sawa na hayo katika eneo hilo hilo.