Kesi ya kifo cha Jeff Mwathi imesukumwa hadi Machi mwaka ujao

Mamake Jeff, Anne Mwathi alikuwa tayari kuendelea na ushahidi wake siku ya Jumatano.

Muhtasari

• Anne Mwathi ambaye alikuwa tayari kuendelea na ushahidi wake siku ya Jumatano, alielezea kusikitishwa kwake akisema sasa amepata maumivu maradufu baada ya kusafiri kutoka Qatar na kukosa kutoa ushahidi.

• Awali kesi hiyo iliposikilizwa, mahakama ilisema itahakikisha kesi hiyoingesikilizwa Novemba 1,2023 saa 9.30 asubuhi.

Kesi ya Jeff kusikilizwa mwaka ujao
Kesi ya Jeff kusikilizwa mwaka ujao

Mamake Jeff Mwathi amelalamikia kuchelewa kusikilizwa kwa kesi ya kifo cha mwanawe baada ya mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Anne Mwathi ambaye alikuwa tayari kuendelea na ushahidi wake siku ya Jumatano, alielezea kusikitishwa kwake akisema sasa amepata maumivu maradufu baada ya kusafiri kutoka Qatar na kukosa kutoa ushahidi.

Hata hivyo, ushahidi wake haukuweza kupokelewa kwa vile wakili wake Danstan Omari hakuwepo, jambo ambalo hakimu mkuu wa Milimani Zainab Abdul, alimkumbusha.

Awali kesi hiyo iliposikilizwa, mahakama ilisema itahakikisha kesi hiyo  ingesikilizwa Novemba 1, 2023 saa tatu unusu asubuhi.

Mawakili wengine akiwemo wakili wa DJ Fatxo, Duncan Okatch, asubuhi walipokea simu kutoka kwa Omari akiwaomba wamwie radhi kwa kuwa bado alikuwa Mombasa na angefika saa 11.30 asubuhi.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, 2024.

Jeff alifariki Februari 23,2023 katika ghorofa ya Redwood, fununu zilidai kuwa aliruka kutoka ghorofa ya 10 nyumbani kwa DJ Fatxo.

Mnamo Agosti, mahakama iliambiwa kwamba Jeff alijaribu kujiua mara mbili kabla ya kifo chake mnamo Februari 23.

Akiwa na msimamo dhabiti, mjombake Jeff, Muchoki Mwathi alipuuzilia mbali madai kwamba mtoto wao alijiua.

Muchoki alikuwa akiongozwa katika ushahidi wake na wakili Omari.

Alisema Jeff anayemfahamu hawezi kujiua kwa sababu mbali na kuwa mjomba wake walikuwa marafiki wa karibu sana ambao walishirikiana sana.

"Kutokana na video hiyo, niliona mwili wa Jeff ukigunduliwa baada ya Fatxo kuondoka saa moja  baadaye. Kama familia tumepoteza mtoto wa kiume ambaye alikuwa na mustakabali mzuri mbele yake," Muchoki alitoa ushahidi mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Zainab Abdul.

Wakili Okatch anayemwakilisha Fatxo alijaribu kudhibitishia mahakama kwamba Jeff alijitoa uhai kwa sababu ya uhusiano mbaya kati ya wazazi wake lakini Muchoki alisema haamini kwamba masuala ya familia yalichangia kifo cha Jeff.

Wakili huyo aliongeza kuwa kuna mashahidi ambao watatoa ushahidi kwamba Jeff alitaka kujiua kwa sababu ya uhusiano kati yake na wazazi.

Hata hivyo, Muchoki alisema kuwa hajui uhusiano wa Jeff na DJ Fatxo lakini wakati mmoja alimwambia Fatxo amempa duka la kubuni na walitakiwa kufanya hivyo pamoja.

Upande wa mashtaka utaita mashahidi 34 kutoa ushahidi.