MCAs wa Kiambu wamtaka gavana ajirekebishe au wambandue ofisini

MCA walitoa makataa ya siku 21 kwa Wamatangi kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Muhtasari

• Katika kikao na wanahabari, wakiongozwa na MCA wa Wadi ya Kikuyu Kamau Boro walimkashifu Gavana  kwa madai ya kulegea katika uongozi.

• “Gavana anasimamia masuala ya Kaunti  pekee bila kujumuisha  bunge la Kaunti katika uangalizi, uwazi na uwajibikaji,”

Gavana wa Kiambu,Kimani Wamatangi
Gavana wa Kiambu,Kimani Wamatangi

Baadhi ya Wawakilishi Wadi wa Kiambu wamemtaka gavana wao Kimani Wamatangi kubadilika na kutishia kuwawasilisha hoja ya kumwondoa madarakani asipofanya vile.

Mnamo Jumatano, MCAs hao walisema wana sababu za kutosha kuwasilisha notisi ya kushtakiwa kwa Wamatangi.

Katika kikao na wanahabari, wakiongozwa na MCA wa Wadi ya Kikuyu Kamau Boro walimshtumu Gavana  kwa madai ya kulegea katika uongozi.

“Gavana anasimamia masuala ya Kaunti  pekee bila kujumuisha  bunge la Kaunti katika uangalizi, uwazi na uwajibikaji,” alidai akisoma taarifa.

Miradi ya maendeleo hasa ya barabara ilitajwa na MCA hao, wakieleza kuwa mwaka jana wa fedha, licha ya kupitishwa kwa bajeti yao, kulikuwa na uboreshaji mdogo sana wa uwepo wa barabara, na kubainisha kuwa bado iko katika hali mbaya.

Kutokana na hali hiyo, MCA walitoa makataa ya siku 21 kwa Wamatangi kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake,wakitishia kumng'oa mamlakani iwapo atafeli kutekeleza ombi lao.

Mnamo Agosti, MCA hao hao walimshutumu gavana Wamatangi kwa udikteta, uongozi uliofeli na kutokuwa na uwezo wa kusimamia mpango wa maendeleo wa kaunti.

Kiini cha malumbano kati ya bunge la kaunti na mawaziri wa kaunti ni madai kwamba Wamatangi alishindwa kuunda serikali yake kikamilifu kwa ajili ya utoaji huduma bora, mwaka mmoja baada ya kushika wadhifa huo.

Wawakilishi hao walidai kuwa tangu  Wamatangi ashike wadhifa wa uongozi, hawezi kueleza miradi ambayo ametekeleza isipokuwa usambazaji wa vifaranga  na mbolea kwa wakulima.

Lakini katika jibu la haraka, Gavana Wamatangi alishikilia kuwa hatatishwa na matakwa ya wafisadi wanaodai kwamba vita katika bunge hilo ni njama ya mahasimu wake wa kisiasa ambao wanapinga mtindo wake wa uongozi na hadhi ya kisiasa.