Mwaliko wa Raila katika dhifa ya kumkaribiasha Mfalme kwenye Ikulu wazua gumzo

Odinga amekuwa na msukumo wa kutaka viongozi wa ODM walienda Ikulu wafurushwe kutoka chama hicho.

Muhtasari

• Kiongozi huyo wa Azimio alionekana akiwa na mazungumzo na mshauri wa usalama wa Rais William Ruto Monica Juma kwenye hafla hiyo

• Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kitaifa,Opiyo Wandanyi,alisita kujadili uwepo wa Odinga kwenye Ikulu alipopigiwa simu na Gazeti la Star.

Raila Odinga kwenye dhifa ya ikulu
Raila Odinga kwenye dhifa ya ikulu
Image: Facebook

Kuwepo kwa kiongozi wa Upinzani Raila Odinga katika hafla ya Ikulu mnamo Jumanne umezua gumzo huku Wakenya   wakikisia iwapo ni njia mojawapo ya kuridhiana na Rais Ruto.

Raila ambaye alikuwa ameandamana na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alikuwa miongoni mwa wageni wakati wa dhifa ya serikali iliyoandaliwa kwa heshima ya  Mfalme Charles III na Malkia Camilla.

Kiongozi huyo wa Azimio alionekana akiwa na mazungumzo na mshauri wa usalama wa Rais William Ruto Monica Juma kwenye hafla hiyo.

Baadaye, alitambulishwa kwa Mfalme na Rais william Ruto baada ya kuwa na kupiga gumzo na baadhi ya mawaziri.

Ikumbukwe kuwa  Raila ameendelea kushikilia msimamo wake kwamba alishinda uchaguzi wa urais wa 2022 na kwamba hawezi kumtambua Ruto kama rais.

Kinara  huyo wa Azimio amekuwa na msukumo wa kutaka baadhi ya wabunge wa ODM ambao hivi karibuni walionekana wakiwa na Rais katika Ikulu wafurushwe kutoka chama hicho.

Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kitaifa,Opiyo Wandanyi,alisita kujadili uwepo wa Odinga kwenye Ikulu alipopigiwa simu na Gazeti la Star.

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alikanusha ripoti kwamba Raila alialikwa na Ruto akisisitiza kuwa alikuwa pale kama rafiki wa familia ya Kifalme.

Osotsi alidai kuwa Raila alikuwa Ikulu kupitia mwaliko wa Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini Kenya Neil Wigan.

“Mnakumbuka Raila alitembelewa na balozi mpya nchini Kenya Oktoba 12...huo ndio wakati kamili alipopokea mwaliko rasmi wa hafla ya kukutana na Mfalme,” alieleza.

Seneta wa Murang'a Joe Nyutu anasema uamuzi wa kumwalika kiongozi huyo ulikuwa wa makusudi na Wakenya hawafaikuuona kwa njia ingine.

Alisema iwapo Ruto angekosa kualika Upinzani, cheche zingerushwa kwamba mazungumzo yanayoendelea hayana matunda.

"Raila sio tu kuungwa mkono na Wakenya lakini pia anatambulika katika mataifa ya Magharibi. Je, ni njia gani bora zaidi kwa Rais Ruto kuonyesha kwamba Kenya imeungana kuliko kuwa na Raila aliyealikwa Ikulu wakati wa ziara ya Kifalme?" alisema.

Mbunge wa Mbeere Kaskazini , Geoffrey Ruku amedai kuwa  huenda Raila alialikwa Ikulu na Balozi wa Uingereza nchini Kenya na si  Rais Ruto.