Ann Waiguru ashukuru seneti kwa kumuokoa gavana Mwangaza

Alimpongeza Mwangaza kwa kuwa jasiri wakati wa kesi iliyomkabidhi

Muhtasari

•Akitoa ushauri kwa Gavana mwenzake wa kike, Waiguru alimtaka Mwangaza kuzingatia kuwaongoza wakazi wa Meru kwa utoaji huduma

•Viongozi kadhaa wanawake walijitokeza Bungeni kusherehekea ushindi wa Mwangaza

Gavana Ann Waiguru awapongeza maseneta kwa kumrudisha Kawira madarakani
Gavana Ann Waiguru awapongeza maseneta kwa kumrudisha Kawira madarakani

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ann Waiguru amewapongeza Maseneta kwa kuchagua kumpa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza nafasi nyingine ya kutawala kaunti hiyo.

Katika taarifa yake Alhamisi, Waiguru ambaye pia ni Gavana wa Kirinyaga aliwapongeza maseneta hao kwa kupiga kura wakiwa na dhamira ya kumpedekeza Kawira arudi madarakani.

"Kwa maseneta wanaowakilisha kaunti 47, asanteni  kwa kupiga kura kwa dhamiri zenu," alisema.

Akisherehekea ushindi wa Mwangaza, Waiguru alimpongeza kwa kuonyesha uso wa kijasiri wakati wote wa kesi yake.

"Hakika - Asiye na wake ana Mungu, wakati wa changamoto na mabishano ndio nguzo ya kweli ya uongozi," alisema.

Akitoa ushauri wake Gavana wa  kaunti ya Kirinyaga alimtaka  Mwangaza  kuwaongoza wakazi wa Meru kwa utoaji huduma.

"Kwa dada yangu Gavana Kawira Mwangaza, ni  kwa sasa ujasiri wa kuendelea mbele na kwa umakini  kutumikia kaunti yako ndio muhimu," Waiguru alisema.

 

Bunge la Seneti lilitupilia mbali mashtaka yote katika kura, na hivyo kumpa Mwangaza maisha mapya katika uongozi wa kaunti.

Alikabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali, upendeleo, uonevu, uteuzi usio halali, kudharau mahakama, na kuipa barabara jina la mumewe kinyume cha sheria.