Kenya yakaribia kumaliza ulipaji wa awamu ya kwanza ya Eurobond - Ruto

"Tumejitahidi sana ndani na nje ya nchi kushauriana na washirika wetu wa maendeleo ili kukomboa nchi yetu kutoka kwenye lindi la madeni."

Muhtasari

• Ruto alisema kuwa baada ya kushika wadhifa wa urais, utawala wake ulilazimika kufanya maamuzi magumu ya kiuchumi ili kudhibiti hali ya uchumi wa taifa.

Rais William Ruto akitoa hotuba yake kwa taifa mnamo Novemba 9, 2023. Picha: BUNGE LA KITAIFA
Rais William Ruto akitoa hotuba yake kwa taifa mnamo Novemba 9, 2023. Picha: BUNGE LA KITAIFA

Rais William Ruto ametangaza kuwa Kenya mnamo Desemba mwaka huu itakuwa imekamilisha ulipaji wa awamu ya kwanza ya Eurobond ya Dola bilioni mbili (Ksh.304B), ambayo ni kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 300 (Ksh.45.6 bilioni).

 

Akitoa Hotuba yake katika bunge Rais William Ruto alisema kuwa baada ya kushika wadhifa wa urais, utawala wake ulilazimika kufanya maamuzi magumu ya kiuchumi ili kudhibiti hali ya uchumi wa taifa ambayo ilikuwa imedorora. Juhudi hizi, alisema, hatimaye zimeanza kuzaa matunda.

 

"Tumejitahidi sana ndani na nje ya nchi kushauriana na washirika wetu wa maendeleo ili kukomboa nchi yetu kutoka kwenye lindi la dhiki ya madeni na kutuweka leo kwenye njia thabiti ya ukuaji wa uchumi endelevu," alisema rais.

Rais aliongeza kuwa kutokana na juhudi thabiti na endelevu za Kenya kulipia deni lake la umma linalozidi kushamiri, uhusiano wa Nairobi na mashirika ya kimataifa ya kutoa mikopo kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika umeimarika.

 

"Lazima tukubali kwamba kama nchi tumekuwa tukiishi maisha ghali kupita uwezo wetu. Wakati umefika wa kuacha starehe za uwongo na matumizi mabaya na ruzuku isiyo na manufaa kwenye matumizi na kujichimbia ndani ya shimo la madeni ambayo tungeepuka," Ruto alisema.