Niko tayari kwa kuvunjwa kwa Kaunti ya Meru - Mwangaza

Mwangaza alisisitiza kwamba ataondoka akijua kwamba alijitahidi kadiri awezavyo.

Muhtasari

•Zaidi ya wakazi 15 wa Meru siku Jumatano waliwasilisha ombi la kutaka kuwafurusha mawaziri wa kaunti. 

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza
Gavana wa Meru Kawira Mwangaza

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amesema  kuwa yuko tayari  kwa wito unaotolewa kuvunjwa kwa kaunti hiyo ili uchaguzi mpya ufanyike.

Gavana huyo alisema kuwa  atazingatia maombi ya wakaazi wa Meru ikiwa wameona inafaa kaunti hiyo kuvunjwa.

"Kuna mashirika kadhaa ambayo yameanza kukusanya saini za kuvunja kaunti baada ya kuona mwelekeo ambao wakilishi wadi wetu wamechukua... nikiwa Gavana, niko tayari kuunga mkono azma yao," Mwangaza alisema.

Bosi huyo wa Kaunti alisisitiza kuwa ataunga mkono wakazi wa Meru ikiwa kwa kuvunja kaunti hiyo watapata usaidizi.

Akitafakari kuhusu miezi 14 aliyokaa ofisini, Mwangaza alisisitiza kwamba ataondoka akijua kwamba alijitahidi kadiri awezavyo.

"Nimefanya kadiri ya uwezo wangu katika mwaka mmoja uliopita kukiwa na misukosuko mingi hakuna gavana mwingine ambaye ameshtakiwa mara tatu katika kipindi cha mwaka mmoja," alisema.

Gavana Mwangaza alibainisha kuwa licha ya matatizo aliyokumbana nayo, alifanikiwa kufanyia kazi kwa wakazi wa Meru na kutekeleza bajeti ya asilimia 72.

Akiwa na matumaini, gavana huyo alisema anajua kuwa atachaguliwa tena ikiwa ni mapenzi ya wakazi wa Meru.

“Kama Mungu ataona vyema na wakazi pia kusema nimefanya kazi, najua nitachaguliwa tena,” Mwangaza aliongeza.

Wiki jana, Seneti ilimuondolea lawama Gavana huyo dhidi ya mashtaka yote saba yaliyokuwa yakimwandama. 

Seneti ilitupilia mbali mashtaka yote dhidi ya Mwangaza, hivyo kumpa maisha mapya katika uongozi wa kaunti.

Alikabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali, upendeleo, uonevu, uteuzi usio halali, kudharau mahakama, na kuipa barabara jina la mumewe kinyume cha sheria.

Gavana Mwangaza alikanusha mashtaka yote na kutoa utetezi mkali akisema alidhulumiwa kama kiongozi mwanamke.

Ombi lingine la kumtimua kutoka Meru lilifikishwa kwa Bunge la Kaunti.

Zaidi ya wakazi 15 wa Meru Jumatano waliwasilisha ombi la kutaka kuwashtaki wajumbe wa kamati kuu ya Baraza la Mawaziri la Gavana Kawira Mwangaza kwa madai ya kukiuka Katiba na sheria.