Wakalenjin wanatawala kazi 184,876 katika kaunti - NCIC

Wakalenjin wamechukua asilimia 15.83 ya jumla ya ajira 184, 876 katika kaunti 47.

Muhtasari

• Wakalenjin wamefuatwa kwa karibu na jamii ya Wakikuyu ambao wamechukua asilimia 15.77 ya ajira kisha Waluhya (asilimia 11.6), Wajaluo (asilimia 9.81), Wakamba (asilimia 8.88), Wakisii (asilimia 7.68), Meru (asilimia 4.88) na Mijikenda (asilimia 4.60).

Kamishna wa NCIC Wambui Nyutu akiwa nje ya afisi ya kamishna wa kaunti ya Garissa Jumatano. Picha: MAKTABA
Kamishna wa NCIC Wambui Nyutu akiwa nje ya afisi ya kamishna wa kaunti ya Garissa Jumatano. Picha: MAKTABA

Watu kutoka jamii ya Wakalenjin wamechukua nafasi nyingi za kazi katika kaunti, utathmini wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano unaonyesha.

Ukaguzi huo, ambao ulitaka kuthibitisha uzingatiaji wa usawa wa kikabila katika nafasi za ajira kwenye kaunti, ulionyesha Wakalenjin wamechukua asilimia 15.83 ya jumla ya ajira 184, 876 katika kaunti 47.

Wakalenjin wamefuatwa kwa karibu na jamii ya Wakikuyu ambao wamechukua asilimia 15.77 ya ajira kisha Waluhya (asilimia 11.6), Wajaluo (asilimia 9.81), Wakamba (asilimia 8.88), Wakisii (asilimia 7.68), Meru (asilimia 4.88) na Mijikenda (asilimia 4.60).

"Inasikitisha kutambua kwamba makabila 29 yanachukua asilimia moja pekee ya kazi. Hili ni jambo la kushangaza, halijumuishi," alisema Kamishna Danvas Makori.

Kamishna Wambui Nyutu hata hivyo alibainisha kuwa kaunti zimepiga hatua katika kuajiri wanawake.

"Ukaguzi ulionyesha jumla ya wafanyakazi 184, 876, asilimia 53 ni wanawake. Kuhusu ajira za wanawake, hatuna malalamishi," Nyutu aliongeza.

Nairobi ina idadi kubwa zaidi ya wafanyikazi 13, 510 ikifuatiwa na Kakamega (7,087) na Bungoma (6,477).

Kamishna wa NCIC Abdulaziz Farah alisema utafiti huo ulifanywa kwa sababu Wakenya wamekumbana na ubaguzi na ukosefu wa usawa hali iliyoendelezwa na wakoloni na serikali zilizofuata.

Farah alisema utafiti huo ulifanywa katika maadhimisho ya miaka 10 ya ugatuzi ili kubaini iwapo kuna mafanikio yaliyopatikana tangu kaunti kuwepo.

"Tatizo letu kuu kama nchi ni mgawanyo usio sawa wa rasilimali. Jambo hili limekita mizizi sana katika kaunti," alisema.

Farah alibainisha kuwa kaunti ya Garissa ndiyo kaunti pekee ambayo haikuzingatia ombi la kutoa data ya uajiri.

Alibainisha kuwa tofauti ni pamoja na utamaduni, rangi, kabila, jinsia na dini.