Mbunge Koech amtaka rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa makini na kauli zake

Haya yanajiri baada ya Uhuru kumsuta Rais William Ruto kwa kumlaumu kwa kushindwa kwa serikali yake na uchumi duni.

Muhtasari

• Akuzungumza siku ya Jumatatu, Koech alimshutumu Uhuru kwa kuelekeza  taifa  katika hali mbaya ya kiuchumi.

• Koech alimtaka Uhuru  aepuke kujihusisha na  siasa badala yake kufuata mambo mengine katika kustaafu kwake.

mBUNGE NELSON KOECH NA ALIYEKUWA RAIS UHURU KENYATTA
mBUNGE NELSON KOECH NA ALIYEKUWA RAIS UHURU KENYATTA
Image: SCREENGRAB

 Mbunge wa Belgut Nelson Koech amemtaka aliyekuwa Rais, Uhuru kenyatta kuwa mwangalifu na matamshi yake kwa umma.

Haya yanajiri baada ya matamshi ya Uhuru wakati wa ibada ya Jumapili mjini Mwingi, Kaunti ya Kitui, ambapo alimsuta Rais William Ruto kwa kumlaumu kwa kushindwa kwa serikali yake na uchumi duni.

“Sitaki kusema mengi… si kwa sababu ninaogopa…niliacha kuogopa. Tumetishiwa, tumeambiwa mambo mengi. Kila mtu anaposhindwa, husema ‘Oh! Serikali iliyopita,” Uhuru aliwaambia waumini.

“Kesho wanawake wakikosa kujifungua watasema ‘Unajua Uhuru alifanya hivyo’. Sijui, lakini nimezoea," aliongeza.

Akizungumza kwenye  runinga ya Citizen siku ya Jumatatu, Koech alimshutumu Uhuru kwa kuelekeza  taifa  katika hali mbaya ya kiuchumi, akimwambia aepuke kukengeusha lawama zozote zinazotolewa dhidi yake na serikali ya Ruto.

“Ili Uhuru ajitokeze kwa ujasiri jana na kusema ‘usinilaumu’ basi anatakiwa kuwa makini sana kwa kauli anazozitoa, tunaumia kwa sababu yake, ni rais tutataka kumsahau,” alisema. Koech.

Koech alimtaka Uhuru  aepuke kujihusisha na  siasa badala yake kufuata mambo mengine katika kustaafu kwake.

"Aende akaketi pale alipo na asitoke nje na kuwakumbusha Wakenya jinsi alivyokuwa na watu wanapiga makofi wakati Kenyatta anawaambia kuwa bado yeye ndiye aliyepanga kushindwa kwa nchi hii."

Matamshi ya Kenyatta, yanajiri wakati viongozi wa kisiasa hasa wa mrengo wa Kenya Kwanza wameonekana wazi wakilaumu serikali iliyopita kwa utendakazi mbaya.

Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua kwa nyakati chache wameeleza kuwa changamoto zilizopo ambazo Wakenya wanakumbana nazo zimechangiwa na kushindwa kwa utawala wa Uhuru.

Viongozi wengine pia wameelekeza lawama kwa serikali iliyotangulia akiwemo Waziri wa Uchukuzi  Kipchumba Murkomen ambaye mnamo Novemba 14, mvua kubwa iliponyesha na kusababisha uvujaji wa paa za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), alisema kuwa hali mbaya ya uwanja wa ndege wa kimataifa, ni kutokana na kazi duni wakati wa uongozi wa Uhuru.