Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kesi ya mauaji ya Daniel Muthiani almaarufu Sniper mnamo Ijumaa walifanikiwa kupata gari lililodaiwa kutumiwa katika utekaji nyara wa mwanablogu huyo wa Meru aliyeuawa.
Katika ripoti ya Jumamosi asubuhi, idara ya uchunguzi wamakosa ya jinai ilifichua kuwa gari hilo aina ya Toyota Premio lenye nambari za usajili KCR 742N lilipatikana katika eneo la Kithoka kaunti ya Meru.
Gari hilo lilidaiwa kutumiwa kumteka nyara marehemu Muthiani na baadaye kutumika kuutupa mwili wake katika mto Mutonga eneo la Chiakariga eneo la Tharaka Nithi mnamo Desemba 2, 2023.
"Kutambuliwa na kupatikana kwa gari hilo, nambari ya usajili ya KCR 742N ya Toyota Premio, KCR 742N, kulifuata uchunguzi wa kina wa njia muhimu, ambazo zilielekeza makazi katika eneo la Canopy, Kithoka, kaunti ya Meru," DCI ilisema katika taarifa.
"Katika taarifa za hivi punde, timu ya wapelelezi imemtambua Vincent Mureithi Kirimi almaarufu Supuu kuwa dereva aliyekodi gari siku ya utekaji nyara na mauaji ya kikatili ya Sniper, likiwabeba watu wengine watatu waliokuwa ndani yake akiwemo Brian Mwenda, Christus Manyara Kiambi na Boniface Kithinji Njihia. DJ Kaboom,” taarifa hiyo ilisomeka zaidi.
Wapelelezi hao walisema wanaendelea na uchunguzi ili kuhakikisha kuwa haki ya mwanablogu wa Meru aliyeuawa inapatikana.
Kesi ya washukiwa wawili wa mauaji ya mwanablogu huyo liliahirishwa wiki iliyopita kwa wiki moja.
Hii itaruhusu upande wa mashtaka kufanya vipimo mbalimbali kwa watuhumiwa.
Supuu na Murangiri Kenneth Guantai almaarufu Tali walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu kuhusiana na mauaji ya Sniper.
Timu ya mashtaka, hata hivyo, iliwasilisha ombi mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Kiambu Jackline Karani, ikitaka kuahirisha ombi hilo kwa siku saba kusubiri uchunguzi wa kiakili wa washukiwa.