Raia 4 wa Nigeria wakamatwa baada ya rapa kuanguka kutoka ghorofa ya 5 na kufariki Riruta

Marehemu alisikika akipiga kelele huku akivua nguo na kuruka kutoka ghorofa ya tano hadi ghorofa ya chini.

Muhtasari

•Charles Waga Otieno anasemekana kuruka kutoka orofa ya tano ya jumba la ghorofa baada ya ugomvi na Wanigeria wanne.

•Waga alikimbizwa katika Hospitali ya Coptic ambako alitangazwa kuwa amefariki alipofika, polisi walisema.

Marehemu Charles Waga Otieno
Image: HISANI

Maafisa wa upelelezi wanawashikilia wanaume wanne raia wa Nigeria kuhusiana na kifo cha mwanamume mwenye umri wa miaka 25 katika eneo la Riruta, Nairobi.

Mwathiriwa aliyetambuliwa kama Charles Waga Otieno anasemekana kuruka kutoka orofa ya tano ya jumba la ghorofa baada ya ugomvi na Wanigeria wanne.

Waga alikuwa rapper chipukizi, marafiki zake walisema.

Wanne hao walikuwa wakaaji wa jumba hilo la ghorofa.

Polisi walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa mwanamume huyo alikuwa ameenda kupeleka zulia katika nyumba hiyo katika ghorofa ya saba, chumba cha 56 kilichokodiwa na Mnigeria ambaye alimlipa Sh400 kwa kazi hiyo.

Baadaye marehemu alisikika akipiga kelele huku akivua nguo na kuruka kutoka ghorofa ya tano hadi ghorofa ya chini ambapo alipata majeraha makubwa kichwani.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Coptic ambako alitangazwa kuwa amefariki alipofika, polisi walisema.

Wanigeria hao wanne walikamatwa wakisubiri uchunguzi wa tukio hilo.

Polisi walisema wanachunguza tukio la mauaji.

Haijabainika ni nini kilimsukuma mwanamume huyo kuruka hadi kukumbana na kifo chake akiwa uchi katika kisa hicho cha Jumatatu alasiri.

Mwili huo ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa maiti.