"Nimehuzunishwa sana!" Eliud Kipchoge aomboleza kifo cha mshindani wake Kelvin Kiptum

Kipchoge alimuomboleza Kiptum kama nyota chipukizi na kusema amehuzunishwa na kifo chake cha kutisha.

Muhtasari

•Eliud Kipchoge ameungana na Wakenya wengine kuomboleza kifo cha bingwa wa mbio za marathon Kelvin Kiptum aliyefariki Jumapili usiku.

•Marehemu aliandikisha rekodi mpya kwa kuchukua sekunde 34 chini ya rekodi ya awali ya Eliud Kipchoge ya saa 2:1:09.

amemuomboleza marehemu Kelvin Kiptum
Eliud Kipchoge amemuomboleza marehemu Kelvin Kiptum
Image: HISANI

Mwanariadha mkongwe wa Kenya, Eliud Kipchoge ameungana na Wakenya wengine kuomboleza kifo cha bingwa wa mbio za marathon Kelvin Kiptum aliyefariki Jumapili usiku.

Kiptum ,24, na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki kufuatia ajali mbaya iliyotokea kwenye barabara ya Eldoret-Kaptagat, umbali mfupi sana kutoka kijiji chake cha Chepsamo, magharibi mwa Kenya.

Katika taarifa yake Jumatatu asubuhi, Kipchoge alimuomboleza Kiptum kama nyota chipukizi na kusema amehuzunishwa na kifo chake cha kutisha.

"Nimehuzunishwa sana na kifo cha mshikilizi wa Rekodi ya Dunia ya Marathon na nyota anayechipukia Kelvin Kiptum," Kipchoge alisema kupitia mtandao wa kijamii.

"Yeye ni mwanariadha ambaye alikuwa na maisha yote mbele yake kufikia ukuu wa ajabu," aliongeza.

Mshikilizi huyo wa zamani wa rekodi ya dunia ya marathon pia alichukua fursa hiyo kufariji familia ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 aliyevunja rekodi yake ya awali.

“Natoa rambirambi zangu za dhati kwa familia yake changa. Mungu awafariji wakati huu wa majaribu,” Kipchoge aliandika.

Kiptum alivunja rekodi ya dunia ya marathon mwezi Oktoba, mwaka jana alipokimbia kwa saa 2:00:35 katika Chicago Marathon, na kuwa mwanariadha wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili na dakika moja.

Marehemu aliandikisha rekodi mpya kwa kuchukua sekunde 34 chini ya rekodi ya awali ya Eliud Kipchoge ya saa 2:1:09.

Huku akimuomboleza marehemu Kiptum siku ya Jumatatu asubuhi, rais William Ruto alimtaja kama nyota aliyevunja vizuizi ili kupata rekodi hiyo ya marathon.

“Kelvin Kiptum alikuwa nyota. Bila shaka ni mmoja wa wanamichezo bora zaidi duniani waliovunja vizuizi ili kupata rekodi ya mbio za marathon,” Rais Ruto aliomboleza.

Aliongeza, "Alikuwa na umri wa miaka 24 tu, kama shujaa, alishinda Valencia, Chicago, London na katika mashindano mengine ya juu. Nguvu zake za kiakili na nidhamu hazilinganishwi. Kiptum ilikuwa mustakabali wetu.”

Amri jeshi mkuu alibainisha kwamba licha ya kufariki akiwa na umri mdogo sana, marehemu Kiptum ameacha alama kubwa sana duniani.

Pia alichukua fursa hiyo kuifariji familia ya bingwa huyo wa mbio za marathon na wadau wote wa tasnia ya michezo.

"Mwanaspoti wa ajabu ameacha alama ya ajabu duniani. Mawazo yetu yako kwa familia na udugu wa michezo. Pumzika kwa Amani,” alisema.