ODM yaahirisha uchaguzi wa mashinani katika kaunti nne

ODM kimeahirisha kwa muda uchaguzi katika kaunti nne, kutokana na mafuriko yanayoendelea.

Muhtasari

• Mnamo Aprili 30, chama hicho kingehitimisha awamu ya kwanza ya zoezi hilo kwa uchaguzi katika kaunti za Kisii, Vihiga na Murang'a.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga (wa tatu kushoto), Mwakilishi wa Wanawake wa Kwale Fatuma Masito na Seneta wa Kwale Issa Boi (kulia) wakicheza katika uwanja wa Kwale Baraza Park katika kaunti ndogo ya Matuga mnamo Alhamisi, Januari 25, Picha: SHABAN OMAR
Kiongozi wa ODM Raila Odinga (wa tatu kushoto), Mwakilishi wa Wanawake wa Kwale Fatuma Masito na Seneta wa Kwale Issa Boi (kulia) wakicheza katika uwanja wa Kwale Baraza Park katika kaunti ndogo ya Matuga mnamo Alhamisi, Januari 25, Picha: SHABAN OMAR

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeahirisha kwa muda uchaguzi katika kaunti nne, kutokana na mafuriko yanayoendelea. 

Katika taarifa ya Ijumaa, mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uchaguzi (NECC) Emily Awiti alisema hii inafuatia maombi ya wanachama  kutoka kaunti hizo wakitaka ratiba ya uchaguzi huo ibadilishwe. Kaunti zilizoathiriwa ni pamoja na Busia, Siaya, Kajiado na Wajir. 

"Sehemu kubwa za kaunti husika zinakabiliwa na mafuriko na changamoto zinazohusiana na mvua zinazoendelea kunyesha," alisema. 

"Baada ya kukagua hali ya msingi na kutathmini maombi, NECC ingependa kutangaza kwamba uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 27, 29 na 30 Aprili, 2024 umeahirishwa kwa muda. Utaendelea mara tu hali itakapoimarika." 

Awamu ya kwanza ya uchaguzi wa mashinani wa ODM ilipangwa kuanza Jumamosi. Katika ratiba iliyotolewa na chama hapo awali, kaunti za Kwale, Busia na Siaya zingepiga kura mnamo Aprili 27 kuwachagua viongozi wao huku Kajiado, Migori na Wajir wakichagua viongozi wao Aprili 29.

Mnamo Aprili 30, chama hicho kingehitimisha awamu ya kwanza ya zoezi hilo kwa uchaguzi katika kaunti za Kisii, Vihiga na Murang'a.

IMETAFSIRIWA NA DAVIS OJIAMBO.