Rais William Ruto amewataka Wabunge kupitisha Bajeti ya 2024-25 ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza mjini Meru wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwa Kiwanda cha kusaga Mahindi cha Meru siku ya Alhamisi, Ruto alisema kwamba bajeti hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mwananchi wa kawaida anapata huduma kama vile umeme.
"Hawa waheshimiwa nataka tafadhali niwahakikishieni tafadhali pitisheni budget haraka hawa wakulima wanahitaji stima," alisema.
Rais pia alisisitiza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, lengo kuu litakuwa katika ujenzi wa barabara, kuunganisha umeme na maji.
"Tayari tumeweka mpango wa bajeti yetu," alisema Pia aliangazia juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa kila mfugaji wa maziwa anapata Sh50 kwa lita ya maziwa kuanzia Julai mwaka huu.
Waziri wa fedha Njuguna Ndung’u alisoma bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2024-25 siku ya Alhamisi, katika majengo ya Bunge.