Serikali katika hali ngumu kugharamia bajeti – Waziri Ndung’u

Alisema kukopa kuna kikomo na ongezeko la kodi lina mipaka pia.

Muhtasari

•Hazina ya Taifa imependekeza njia nyingi za kufikia malengo yake ya mapato kugharamia bajeti ya shilingi 3.92 trilioni.
•Serikali inalenga kukusanya shilingi 2.91 trilioni kutoka kwa mapato ya kawaida.

Waziri wa fedha Njuguna Ndung'u
Waziri wa fedha Njuguna Ndung'u akisoma Bajeti Waziri wa fedha Njuguna Ndung'u
Image: Maktaba

Kuongeza kodi ndiyo chaguo pekee muhimu ambalo serikali imesalia nalo inapopiga hatua katika kugharamia matumizi yaliyoongezeka, waziri wa Hazina Njuguna Ndung’u amesema.

Akitoa makadirio ya bajeti ya mwaka 2024-25 katika Bunge la Kitaifa, Ndung’u alinena kuwa serikali inajipata kati ya mwamba na sehemu ngumu inapotarajia kutoa huduma kwa wakenya kufikia shilingi 3.92 trilioni huku vyanzo vya mapato vikiwa vimekabwa.

"Tuna shida moja kuu kwenye awamu tatu. Kuna kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya serikali, ambayo ina maana kwamba lazima tugharamie hayo kupitia ushuru au madeni," alisema.

Waziri alisema kuwa kukopa si chaguo kwa kuwa kuna udhibiti kwa kiasi ambacho serikali inaweza kukopa wakati wowote, hasa kutokana na hali ya kiuchumi inayoshuhudiwa nchini.

Alisema kuwa hali inazidi kuwa segemnege na kuwa  kuongeza kodi ndiyo chaguo pekee kwani vipo vikwazoambavyo serikali inaweza kuongeza kodi bila kuvipita.

"Kuna vidhibiti na hata mipaka iliyowekwa kwa suala la ukusanyaji madeni ya umma na hata uwezo wa uchumi kubeba mzigo wa madeni. Kuna vidhibiti katika suala la kukusanya mapato ya juu ya kodi," alisema Ndung’u.

Bajeti ya mwaka huu ndiyo kubwa zaidi katika historia ya taifa na ya pili tangu Rais William Ruto ashike hatamu.

Hazina ya Taifa imependekeza njia tofauti za kufikia malengo yake ya mapato kugharamia bajeti ya shilingi 3.92 trilioni ikiwa ni pamoja na kuanzisha kodi mpya katika Mswada wa Fedha, 2024.

Kati ya bajeti yote, serikali inataka kutumia shilingi 1.58 trilioni kwa matumizi ya kawaida, shilingi 727.9 bilioni kwa matumizi ya maendeleo, shilingi 1.21 trilioni kwa huduma za mfuko wa pamoja na shilingi 400 bilioni kama mgao wa haki kwa kaunti.

 Serikali inalenga kukusanya shilingi 2.91 trilioni kutoka mapato ya kawaida, sehemu kubwa ikitarajiwa kupitia mapendekezo katika Mswada wa Fedha, 2024, na shilingi 441 bilioni nyingine kutoka kwa makadirio ya wizara kwa msaada.

 Hazina ya Taifa imekadiria upungufu wa shilingi 508.9 bilioni ambapo inatafuta kupata shilingi 257.9 bilioni kwa kukopa kutoka kwa wakopeshaji wa ndani.

 Kiasi kilichobaki cha shilingi 256.7 bilioni kitatolewa kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa.