Wananchi wakosoa pendekezo la kuongeza viongozi mishahara

Malipo haya ya juu yamezusha mdahalo mkali miongoni mwa wakenya

Muhtasari

•Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, vilevile spika wa Seneti Amason Kingi, watabugia kitita cha shilingi 1,208,362 na 1,185,327 mtawalia.

•"Wahudumu wa matibabu wamekuwa nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini tuna pesa za kuongeza mishahara ya wabunge ... unaona shida iko wapi?" alilonga Branice Munyasa.

Bunge la Kenya
Wabunge wapata nyongeza ya mishahara yao Bunge la Kenya
Image: Twitter @NAssembly Kenya

Licha ya wakenya kuisukuma serikali ya Rais William Ruto kupunguza mishahara ya viongozi wa serikali,  wabunge na viongozi wengine wa serikalini wanatarajia kupokea nyongeza ya mishahara yao kuanzia mnamo Juni 1.

Tume ya  kudhibiti Mishahara nchini (SRC) imependekeza nyongeza kwa mishahara ya maafisa wakuu wa serikali maseneti na wabunge katika mwaka wa kifedha 2024/25.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, vilevile spika wa Seneti Amason Kingi, watabugia kitita cha shilingi 1,208,362 na 1,185,327 mtawalia.

Kiongozi wa wengi katika bunge, Kimani Ichung’wah atabugia shilingi 800,019 huku kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi akibugia kitita sawai n Ichung’wah. Wabunge kwa upande mwingine, watapokea shilingi 739,000.

“Muundo wa malipo ya kila mwezi kwa maafisa wa umma kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa yatatekelezwa kwenye mwaka wa kifedha 2024/2025 na utekelezaji huu utaanza mnamo Julai 1, 2024,” ripoti ilisoma.

Malipo haya ya juu yamezusha mdahalo mkali miongoni mwa wakenya ambao wanajikaza kisabuni ili kupata riziki.

Vijana wenye hamaki wamekuwa wakipanga maandamano ya amani kwa maeneo mbalimbali ya huku wakishutumu viongozi waliochaguliwa dhidi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

“Haya ni maajabu. Yaani hata baada ya hotuba ya Rais ya kupunguza matumizi ya mali ya umma wabunge wetu wameamua kuongeza mishahara yao?” Aliuliza Propesa kwenye jukwaa lake la X.

Abdirahman Taqal alisema, "Tunahitaji mawasiliano ya maafisa wa @srckenya..huwezi kukata mishahara ya wahudumu wa afya huku ukiwapa wabunge pakiti nyingi."

"Wahudumu wa matibabu wamekuwa nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini tuna pesa za kuongeza mishahara ya wabunge ... unaona shida iko wapi?" alilonga Branice Munyasa.

Mbali na hayo, baadhi ya wananchi wameibua hisia mbalimbali kwani Rais alikuwa amenena kuwa atapunguza mishahara yake na viongozi wengine serikalini ili kupunguza ubadhirifu wa mali ya wananchi villevile kukomesha ufisadi.