Majonzi maradufu! Mamake mtoto aliyepigwa risasi wakati wa maandamano anyang'anywa mwili aienda kumzika

“Nimenyang’anywa mtoto wangu! Kwa nini nimenyang’anywa mtoto wangu? Kwani hii Kenya tuko Kenya gani?

Muhtasari

•Mipango wa mazishi ya mvulana mwenye umri wa miaka 12 aliyeuawa wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha imetatizwa.

•Waombolezaji wengine waliokuwa na mamake marehemu walisikika wakilalamika pia na kushangaa mwili wa mtoto umefanya nini.

Mamake Kennedy Onyango
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mipango wa mazishi ya mvulana mwenye umri wa miaka 12 aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha imetatizwa.

Mamake marehemu Kennedy Onyango alikuwa amesafiri kutoka Nairobi hadi eneo la Mbita, Kaunti ya Homabay mnamo Ijumaa kwa madhumuni ya maziko lakini kundi la polisi lilidaiwa kuuchukua mwili huo kwa sababu ambazo hazijafichuliwa.

Katika video iliyochapishwa na mchekeshaji Eric Omondi siku ya Jumamosi, mama huyo wa maombolezo aliomba serikali kumsaidia kurejesha mwili wa mwanawe ili aweze kupata ufungo kwa kumzika.

“Jana nilisafiri na mtoto wangu nikiwa nakuja nikijua nitamzika. Mtu akikufa ukimzika ndo unajua umemzika na ndiye huyo hapo na hiyo ndo kaburi lake. Kufika huku Mbita tukanyang’anywa mtoto na maaskari. Hadi saai sijaona mtoto wangu, sijamuona mtoto wangu. Serikali nisaidie nizike mtoto wangu,” mamake Kennedy alilalamika kabla ya kuangua kilio.

Waombolezaji wengine waliokuwa na mamake marehemu walisikika wakilalamika pia na kushangaa mwili wa mtoto umefanya nini.

“Nimenyang’anywa mtoto wangu! Kwa nini nimenyang’anywa mtoto wangu? Kwani hii Kenya tuko Kenya gani? Mpaka unanyang’anywa mtoto wako. Yaani naomboleza mtoto wangu, mwingine ako na roho ya kuninyang’anya. Mungu wangu. Naomba mtoto wangu,” mamake Kennedy aliendelea kulia.

Akielezea hali hiyo, mchekeshaji Eric Omondi ambaye alikuwa ameungana na mamake kwa mazishi yaliyopangwa alisema walipata kizuizi cha barabarani walipokuwa wakisafiri kwenda kumzika mvulana huyo kabla ya mwili kudaiwa kuchukuliwa.

Aliomba mwili urudishwe kwa ajili ya mazishi.

"Kwa hivyo, tulifika Homabay kumzika Kennedy mwenye umri wa miaka 12 na kabla ya kufika nyumbani tulipata kizuizi cha barabarani cha polisi. Wakamchukua yule kijana. Yeyote anayehusika naomba mruhusu mwanamke huyu aomboleze kwa Amani mruhusu amzike Mwanae. Ameteseka vya kutosha,” Eric alisema.

Mtoto  huyo aliyefariki baada ya kudaiwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ambayo yalishuhudiwa hivi majuzi nchini alitambuliwa kwa jina la Kennedy Onyango.

Picha za majeraha ya risasi mgongoni ziliwatia hofu Wakenya kwenye mitandao ya kijamii na walitaka haki itendeke kwa mvulana huyo.

Zaidi ya majeraha 8 ya risasi yalionyesha wakati wa kutisha polisi wa kupambana na ghasia walipompiga risasi.