logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sudi hatimaye azungumza kuhusu uharibifu na uporaji wa klabu yake, Timba XO

Sudi alisema kuwa watu wengi walipoteza kazi zao baada ya kufungwa.

image
na SAMUEL MAINA

Habari06 July 2024 - 07:26

Muhtasari


  • • Sudi amekashifu watu walioharibu mali wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha yaliyotokea nchini kote wiki chache zilizopita.
  • •Alikashifu uharibifu na uporaji uliofanyika katika klabu yake ya Timba XO mjini Eldoret akisema kuwa watu wengi walipoteza kazi zao baada ya kufungwa.
  •  
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amekashifu watu walioharibu mali wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha yaliyotokea nchini kote wiki chache zilizopita.

Akizungumza siku ya Ijumaa wakati wa mazishi ya mtu wa familia katika eneo la Kesses kaunti ya Uasin Gishu, mbunge huyo wa UDA alidai kuwa machafuko ambayo yalishuhudiwa yalipangwa na maadui wa serikali.

Alisema alishtuka sana kuona watu wakiharibu mali hata ambayo haina uhusiano wowote na mswada wa fedha wa 2024 uliokosolewa sana.

“Nilishangaa sana kwanza kuchoma kaunti kama ya Uasin Gishu.Ni jambo lenye aibu sana, tunaonekana wajinga sana kwa sababu Muswada wa Fedha unaingiliana wapi na kaunti? Finance bill inaingiliana wapi na kortini? Finance Bill inaingiliana wapi na bunge? Inaingia wapi na biashara ya watu?,” Sudi alisema.

Mwanasiasa huyo alidai kuwa hata alipokea vitisho kuhusu nyumba yake kuchomwa.

Alikashifu uharibifu na uporaji uliofanyika katika klabu yake ya Timba XO mjini Eldoret akisema kuwa watu wengi walipoteza kazi zao baada ya kufungwa.

“Pale kwangu Timba, sio tu vile watu wanasema eti ni kilabu. Pale kuna maduka, kuna mahali ya kunywa chai, kuna car wash, kuna mahali ya kutengenezea magari na kuna hoteli,” alisema.

Aliongeza, “Tumepoteza wafanyikazi 220 ambao walikuwa wakifanya kazi pale. 220 kama mtu ako na watoto watatu ama watano, hiyo ni kupoteza watu 600 ambao walikuwa wakitegemea pale ukubwa. Lakini kwa ssababu ya ujinga na furaha yako, kusema lazima uchome Timba ndio huyu jamaa asikie. Sasa mimi, unadhani ukichoma Timba utanikata mkono? Unafikiri utanisimamisha mimi Sudi? Mimi niko na historia.”

Sudi aliwakosoa wanaodaiwa kupanga machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano hayo na kuwataka Wakenya kuacha siasa mbovu.  

Mapema wiki hii, iliripotiwa kwamba klabu ya Timber XO, ambayo ilivunjwa na kuporwa wakati wa maandamano ilikuwa imefungwa kwa muda kwa ajili ya ukarabati.

Chanzo kilicho karibu na Mbunge Sudi kilisema klabu hiyo ilikuwa imefungwa kwa ukarabati.

"Klabu imefungwa kwa ajili ya ukarabati na itafunguliwa mara tu ukarabati utakapokamilika," chanzo hicho ambacho hakikutajwa jina kilisema.

Klabu hiyo ilifunguliwa mwezi Mei.

Watu wanaoshukiwa kuwa wahuni waliovamia sehemu hiyo ya burudani waliharibu kuta za vioo, madirisha na milango ya jengo hilo na kutorosha  vileo vya thamani ya maelfu ya shilingi.

Sudi alikuwa tayari ametangaza kuwa atachukua likizo ya mapumziko kutoka kwa shughuli za umma na shughuli za maendeleo.

Alieleza kuwa alichukua uamuzi huo kwa sababu kushiriki kwake katika shughuli kama vile Harambee kumetumika dhidi yake.

“Kusonga mbele sitashiriki Harambee yoyote kwa sababu imekuwa ikitumika kukashifu na kudharau mwenendo mzuri, ipigwe marufuku,” alisema.

Takriban vijana 15 walifikishwa katika mahakama ya Eldoret Jumatatu kuhusiana na maandamano katika mji huo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved