Serikali imepuuzilia mbali madai kuwa kuna njama ya kuuza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa wawekezaji wa kigeni.
Ripoti kuhusu madai ya kuuzwa kwa uwanja huo wa ndege zimetawala mitandao ya habari nchini Kenya na kusababisha maandamano ya Jumanne yaliyopewa jina la 'OccupyJKIA'.
Mkuu wa mawaziri ambaye pia ni kaimu waziri wa uchukuzi Musalia aliambia Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Bajeti kwamba uuzaji wa Uwanja huo unaweza tu kufanywa kupitia idhinisho la bunge.
“Uwanja wa ndege hauuzwi. Hii ni mali ya umma, rasilimali muhimu. Ikiwa ungeuzwa, lazima mchakato kamili wa umma ambao bunge limeidhinisha uzingatiwe,” Mudavadi aliwaambia wabunge.
Alisema kuna mipango ya kubadilisha uwanja wa ndege kuwa wa kisasa na kujenga eneo jipya la mapokezi.
Seneta wa Kisii Richard Onyoka alidai kupata fununu kuhusu uuzaji wa uwanja huo. Anadai serikali imeafikia uamuzi kukabidhi umiliki wa JKIA kwa mwekezaji wa kigeni.
Ripoti za madai ya kuuzwa kwa uwanja huo wa ndege zimechochea maandamano ya kupinga serikali Jumanne hadi JKIA.