Mwandamanaji wa Uganda alikamatwa na maafisa wa usalama siku ya Jumanne asubuhi wakati akielezea madai yao nje ya bunge la taifa.
Mwandamanaji huyo ambaye anaripotiwa kuwa wa kwanza kufika bungeni alikuwa akijaribu kuwasilisha malalamiko yao kwa wanahabari wakati askari waliokuwa na sare walimvamia na kumsindikiza hadi kwenye gari la polisi lililokuwa limesimama karibu.
Yeye ni miongoni mwa waandamanaji vijana nchini Uganda ambao wametishia kuandamana hadi bungeni kupinga utawala mbovu.
“Nipo hapa Bungeni. Tunasema hatutaki ufisadi bungeni. Ufisadi bungeni uko kwa kasi kubwa,”mwandamanaji huyo alisikika akiwaambia wanahabari waliokuwa wakimrekodi.
Alishikilia bango lililoandikwa ‘Stop Corruption in the Parliament of Uganda.’
“Ndiyo niko hapa nimesimama bungeni. Ufisadi sasa uko kileleni. Kila mtu ni fisadi maofisini, RDC, kata, wilaya, kila mahali. Kila kitu ni ufisadi. Niko hapa kuandamana bungeni ili Waganda, ni sauti yetu tutoke,” alisema kabla ya maafisa kadhaa kumvizia na kumsindikiza kwa fujo hadi kwenye gari la polisi lililokuwa likimsubiri.
Waandishi wa habari waliachwa wakimuuuliza mwandamanaji huyo kuhusu madai yao huku akibebwa kwa gari ya polisi haraka.
Haya yanajiri huku vijana katika nchi hiyo jirani wakijaribu kuandamana hadi bunge katika juhudi za kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao.
Miongoni mwa madai yao ni pamoja na;
1.Kupunguzwa kwa idadi ya Wabunge.
2.Kujiuzulu kwa Anita Among kama spika wa bunge.
3.Kupunguza kwa mishahara ya Wabunge hadi Ugx 3m (Ksh106,370).
4.Kukaguliwa kwa mitindo ya maisha ya Wabunge na maelezo kuwekwa wazi.
5.Kujiuzulu kwa Wabunge wote waliohusika katika kashfa yoyote.
6.Kujiuzulu kwa makamishna wanne wa bungeni.
7.Waganda kuruhusiwa kukusanyika kwa amani bila kuzuiwa.