Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Radio Africa Group Martin Khafafa amechukua nafasi ya Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni.
Tangazo hilo lilitolewa na mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Radio Africa Group Kiprono Kittony siku ya Jumatano.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Patrick Quarcoo kustaafu kutoka Radio Africa Group baada ya kuitumikia kwa miaka 24.
Katika tangazo hilo, Kittony alisema hakuna mabadiliko makubwa katika kampuni hiyo.
"Martin Khafafa sasa ndiye Mkurugenzi Mtendaji mpya kuanzia leo na hakuna mabadiliko mengine mapya katika usimamizi," Kittony alisema.
Kittony alipitisha mawasiliano hayo wakati wa tafrija ya kumuaga Mkurugenzi Mtendaji wa zamani Quarcoo ambaye alistaafu kuanzia Julai 24, 2024.
Kittony aliwaomba wafanyakazi wa Radio Africa kumuunga mkono Khafafa anapochukua nafasi hiyo mpya.