Ruto apendekeza Douglas Kanja kuwa IG wa polisi na kuteua manaibu wa IG

Kanja amekuwa akihudumu kama kaimu Inspekta Jenerali wa polisi tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa IG Japhet Koome.

Muhtasari

• Eliud Lagat atakuwa naibu jenerali wa polisi kitengo cha polisi wa kawaida huku Gilbert Misengeli akishikilia kitengo cha polisi wa utawala (AP).

Douglas Kanja
Image: HANDOUT

Rais William Ruto amependekeza Douglas Kanja Kirocho kuwa Inspekta Jenerali wa polisi.

Kanja amekuwa akihudumu kama kaimu Inspekta Jenerali wa polisi tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa IG Japhet Koome.

"Kwa mujibu wa Kifungu cha 245 (2) cha katiba Mheshimiwa Rais amemteua Bw. Douglas Kanja Kirochi kuteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa", waraka wa rais ulisema.

Kanja ana tajiriba ya karibu miongo minne ambapo amepanda kutoka cheo cha chini hadi kufikia aliko sasa. Awali alihudumu kama naibu Jenerali wa polisi, kamanda wa kikosi cha GSU na kamanda wa polisi katika kaunti ya Kilifi.

 

Katika barua kwa tume ya Huduma kwa polisi siku ya Alhamisi Rais Ruto pia aliwateua Eliud Kipkoech Lagat na Gilbert Masengeli kuwa manaibu wa Inspekta Jenerali wa polisi.

Eliud Lagat atakuwa naibu jenerali wa polisi kitengo cha polisi wa kawaida huku Gilbert Misengeli akishikilia kitengo cha polisi wa utawala (AP).