Katika onyesho la ushirikiano, baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wamejikeza kumtetea Naibu Rais Rigathi Gachagua huku ripoti za njama ya kumwondoa madarakani zikizidi.
Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa umoja na utulivu ndani ya serikali na kuapa kukabiliana na mpango wowote wa kumfukuza Gachagua ofisini.
Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba alisema hawatakubali Naibu Rais kudhulumiwa na kunyanyaswa.
Aliwashutumu wafadhili wa njama ya kung’atua ofisini kwa kutaka kuwahadaa Wakenya kutoka kwa masuala muhimu zaidi.
"Wanatafuta tu sababu ya kugeuza mawazo kutoka kwa maandamano yanayoendelea ambayo yanafanyika nchini Kenya ili waweze kuwakabili watu binafsi," alisema.
"Tunasubiri maswala wale wanaotaka kumshtaki Naibu rais, hatutaruhusu mtu yeyote kuwadhulumu wengine kwa sababu ya kutetea na kuwakilisha jamii yao."
Mbunge maalum Sabina Chege pia ameelezea kumuunga mkono DP Gachagua akisema anasimama kidete upande wake.
Sabina Chege alisema bado ni mapema kuwasilisha madai ya kumuondoa madarakani naibu wa Ruto, akiongeza kuwa iwapo Ruto atakuwa na mambo yoyote na naibu wake, anapaswa kujitokeza na kuyasema mbele ya Wakenya.
"Vipaumbele katika hii serikali vimegeuzwa juu chini. Kwa nini ufikirie hoja ya kumfurusha badala ya kufikiria jinsi ya kutatua changamoto katika Bunge na matatizo mengine ambayo Wakenya wanayo," alisema.
Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya, ambaye ni mshirika wa karibu wa Gachagua, amemkashifu mbunge wa Kiambu kwa kuongoza hatua ya kumng'atua DP. Gakuya alisema mbunge huyo amekuwa akiongoza njama hiyo kwa kuongoza ukusanyaji wa sahihi.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, ambaye ni mshirika mkubwa wa Gachagua, kwa upande wake, alithubutu wanaohusishwa na njama hiyo ya kumtimua naibu rais akisema watapatwa na mshtuko mbaya.
Kahiga alitaja kuwa ni bahati mbaya mipango yoyote ya kumwondoa DP madarakani. Kahiga alisema juhudi za baadhi ya viongozi kuwasilisha hoja ya kumtimua Riggy G hazitaona mwanga akisema kwamba shutuma dhidi ya Gachagua ni za kipuuzi.
“Yeyote anayeona hiyo ndiyo njia yake, tunawaambia ailete na tutaishughulikia muda huo ukifika,” alisema. "Nchi inahitaji kutulizwa.
Tumepoteza miaka miwili ambayo imepita kwa sababu ya maandamano ya Gen Z. Tunahitaji kuleta nchi katika utulivu. Tuna Mawaziri ambao wanapaswa kuangaliwa.
Matamshi ya viongozi hao yanajiri wakati idara ya DCI imeanzisha uchunguzi wake kuhusu madai ya wanasiasa kufadhili maandamano ya Gen Z.
Siku ya Jumanne, wasaidizi wakuu watatu wa Gachagua walihojiwa kuhusiana na maandamano hayoBaadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kama mpango wa kumlenga DP kisiasa.