Maafisa wa upelelezi wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 24, aliyetoweka, ulipatikana katika bwawa la Kangemi, Nairobi.
Simon Owino aliripotiwa kutoweka tangu Julai 26. Aliishi katika eneo hilo alipotowekea. Baba yake aliripoti kuwa hapatikani.
Mwili huo uligunduliwa Julai 30 katika bwawa la Kangemi na wenyeji.
Ulikuwa ukielea kwenye bwawa hilo wakati wapiga mbizi waliporuka na kuutoa. Baba ya marehemu alitambua mwili huo kwenye eneo la tukio, polisi walisema.
Wenyeji walilalamikia kifo hicho na kasi ndogo ya polisi kufika katika eneo la tukio.
Waliutoa mwili huo majini na kuupeleka katika barabara ya Waiyaki Way iliyo karibu na kusababisha msongamano wa magari huku wakidai gari la polisi kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Kundi hilo pia lilitaka uchunguzi ufanywe kuhusu kifo cha Owino.
Gari la polisi lilitumwa eneo la tukio ili kuupeleka mwili wa marehemu kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Polisi wa kuzuia ghasia walitawanya kundi hilo kuwezesha magari kusonga.
Uchunguzi wa kifo hicho unaendelea, polisi walisema.
Haijabainika ni nini kilisababisha kifo hicho.
Wenyeji wanashuku kuwa mwathiriwa ni miongoni mwa wale waliolengwa kutokana na maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.