•Ruto alibainisha kuwa Kenya ilikuwa katika hali ya kipekee ambayo ililazimu kuweka kando maslahi ya kibinafsi au ya kisiasa.
•Ruto aliandamana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Ardhi Alice Wahome.
Rais William Ruto ametetea uamuzi wake wa kuwahusisha viongozi wa upinzani katika serikali yake akisema ni muhimu kwa umoja wa taifa.
Ruto ambaye alikuwa akihutubia wakazi wa Kobujoi, eneo la Aldai, kaunti ya Nandi, alibainisha kuwa Kenya ilikuwa katika hali ya kipekee ambayo ililazimu kuweka kando maslahi ya kibinafsi au ya kisiasa.
"Kuna wakati katika ustawi wa taifa ambapo umoja wa taifa, maendeleo ya Kenya, mabadiliko ya taifa letu ni muhimu zaidi kuliko ushawishi wowote wa kisiasa, pande za kisiasa, muundo wa kisiasa au maslahi yoyote ya jamii," alisema. alisema.
"Hata ni zaidi ya maslahi binafsi ya viongozi, lazima tuungane na huo ni wakati kama huu katika nchi yetu," aliongeza.
Ruto aliandamana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Ardhi Alice Wahome.
Magavana Stephen Sang (Nandi) na James Orengo (Kisumu) na wabunge kadhaa pia walikuwepo.
Mkuu huyo wa nchi alibainisha kuwa mabadiliko ya taifa yanawahitaji viongozi wote na Wakenya kwa jumla kuwa na umoja bila kujali misimamo yao ya kisiasa.
Alikuwa katika kaunti hiyo kukagua ujenzi wa soko la Kobujoi.
Inastahili kufunguliwa mnamo Desemba.
Hapo awali, rais alizindua mradi wa usambazaji wa stima katika eneo la Kesogon ambao utahudumia nyumba 6,000.
Serikali, alisema, imetenga Sh330 milioni kwa eneo bunge kwa ajili ya mpango huo.
Wakati uo huo, Ruto alisema wametoa Sh1 bilioni kwa New KCC ili kununua maziwa kutoka kwa wakulima.
Alisema kuanzia mwezi ujao, wakulima watachukua Sh50 kwa kila lita ya maziwa itakayotolewa.