•Kulingana na mmoja wa wanafunzi, Madzao aliwasiliana mara ya mwisho na mkuu wa wafanyakazi wa UNSA mwendo wa saa tatu usiku.
•UNSA sasa inaomba taarifa kuhusu aliko ikisema haijasikia mawasiliano yoyote kutoka kwake tangu wakati huo.
Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UNSA) Rocha Madzao ameripotiwa kutoweka, huku msako ukiwa bado haujazaa matunda yoyote.
Madzao anasemekana kutekwa nyara Ijumaa usiku na watu wasiojulikana alipokuwa akielekea nyumbani kwake.
Kulingana na mmoja wa wanafunzi, Madzao aliwasiliana mara ya mwisho na mkuu wa wafanyakazi wa UNSA mwendo wa saa tatu usiku.
“Alimpigia simu msaidizi wake ambaye ni mkuu wa wafanyikazi akisema alikuwa akinyanyaswa na wanaumekadhaa na baada ya hapo simu yake ilikatika,” alisema.
"Simu hiyo ilikata ghafla baada ya sekunde 23 kabla ya kutaja eneo alikokuwa," aliongeza.
UNSA sasa inaomba taarifa kuhusu aliko ikisema haijasikia mawasiliano yoyote kutoka kwake tangu wakati huo.
"Ikiwa una maelezo yoyote kuhusu Rocha, tafadhali tujulishe," chapisho lililosambazwa lilisomeka.
Mapema siku ya Ijumaa, kikundi kisichojulikana kinadaiwa kujaribu kumkamata bila mafanikio karibu na ukumbi wa 9.
Hii ni baada ya hotuba yake ambapo alitoa makataa ya wiki moja kwa serikali kufutilia mbali mtindo mpya wa ufadhili wa elimu.
"Tunaipa serikali wiki moja kuachana na mtindo huu, tukishindwa kufanya hivyo mnamo Septemba 2," alisema.
Aliongeza "Ninawaomba wanafunzi na wananchi wote wenye mapenzi mema kuungana nasi kwa viatu vizuri vya kucheza na vuvuzela tunapotetea haki yetu ya kupata elimu ya msingi na ya lazima bila malipo kwa kila mtoto."
Siku ya Jumamosi, baadhi ya wanafunzi walifunga barabara kuu ya Uhuru wakipinga kabla ya polisi kutawanyika.
Maandamano hayo yalifuatia "wito wa kuchukua hatua" wa Katibu Mkuu wa UNSA Ramesh Saxena.
"Sote tunajua kuwa rais wa chuo kikuu kukosa hata dakika 10 sio suala la kusubiri," alisema Saxena, akiwataka viongozi wote wa wanafunzi kote nchini kusimama kwa mshikamano hadi rais wa UNSA apatikane," Saxena alisema.